Wakati Uislamu ulipokuwa imara kwa watu, ndipo Allaah akawazidishia imani kwa kugeuza Qiblah kutoka Yerusalemu kuelekea Ka´bah. Amesema:

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ ۖ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا ۚ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza Qiblah unachokiridhia. Hivyo basi, uelekeze uso wako upande wa al-Masjid al-Haraam. Na popote mtakapokuwepo, basi elekezeni nyuso zenu upande wake.”[1]

Walipokuwa Madiynah wakawa wanazungumzishwa kwa jina la imani kila pale wanapoamrishwa au kukatazwa. Wakati alipowaamrisha akasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا

“Enyi mloamini! Rukuuni na sujuduni.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ

“Enyi mlioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi, na panguseni kwa [kupaka maji] vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”[3]

Wakati alipowakataza akasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا الرِّبَا أَضْعَافًا مُّضَاعَفَةً

“Enyi walioamini! Msile ribaa mkizidisha maradufu juu ya maradufu.”[4]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْتُلُوا الصَّيْدَ وَأَنتُمْ حُرُمٌ

“Enyi walioamini! Msiue mawindo na hali mko kwenye ihraam.”[5]

Namna hii ndivo yalivyokuwa maamrisho na makatazo baada ya kuhajiri. Hapo mwanzoni waliitwa hivyo kwa njia ya kukiri peke yake, kwa sababu hakukuweko na faradhi nyenginezo. Polepole Shari´ah ilipokuwa inateremshwa yakawalazimu hayo mengine kama ilivyowalazimu kukiri hapo mwanzoni. Hakuna tofauti kati ya hayo, kwa sababu maamrisho na makatazo yote ni vyenye kutoka kwa Allaah. Wangekataa kuswali kwa kuelekea Ka´bah na wakang´ang´ania na ile imani ya mwanzo, basi isingekuwa na maana yoyote na kungevunjwa kule kukiri kwao. Kwa sababu utiifu wa kwanza hauna haki zaidi ya kuzingatiwa kuwa imani kuliko utiifu wa pili. Wakati walipoitikia amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya swalah kama ambavyo hapo kabla walivokubali kukiri, ndipo wote wakawa waumini. Hivi sasa swalah imeongezwa juu ya jambo la kukiri.

[1] 2:144

[2] 22:77

[3] 5:6

[4] 3:130

[5] 5:95

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 12/05/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy