Dalili ya kuonyesha kuwa swalah ni katika imani ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ

“Allaah hakuwa Mwenye kupoteza swalah zenu.”[1]

Aayah iliteremshwa juu ya wale Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walioswali kuelekea Yerusalemu na wakafa kabla ya kugeuzwa Qiblah. Pindi alipoulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndipo kukateremshwa Aayah hii[2]. Kuna dalili gani nyingine itayotafutwa juu ya kwamba swalah ni katika imani baada ya Aayah hii?

Kitambo fulani wakabaki katika hali hiyo. Walipopokea swalah kwa moyo mkunjufu ndipo Allaah akawafaradhishia zakaah na kusema:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah.”[3]

Wangelitambua zakaah kwa ndimi zao na wakaswali lakini wakati huohuo wakakataa kuitoa, basi yangelibatilishwa yale yote ya kabla yake na kule kukiri kwao swalah kungebatilishwa, kama ulivyokuwa mfano uliotangulia juu ya swalah na kukiri. Haya yanathibitishwa na mapambano ya Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) bega kwa bega pamoja na Muhaajiruun na Answaar dhidi ya wale waarabu waliokataa kutoa zakaah kama ambavo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipambana dhidi ya washirikina. Hakuna tofauti kati yao inapokuja katika kumwaga damu, kuwafunga mateka na kukamata ngawira. Hayohayo yanaweza kusemwa juu ya nembo zengine zote za Uislamu. Kila kunapoteremshwa Shari´ah basi ilikuwa inaongezwa juu ya ile ya kabla yake na ikakusanya imani. Hivyo wale wenye kuitendea kazi wakaitwa kuwa ni “waumini”.

[1] 2:143

[2] al-Bukhaariy kupitia kwa al-Barraa’ na at-Tirmidhiy, kupitia kwa Ibn ´Abbaas, ambaye ameisahihisha.

[3] 02:83

Zakaah imetajwa katika Aayah nyingi zilizoteremshwa kipindi cha Makkah. Mara imetajwa katika hali ya kuamrishwa, wakati mwingine inatajwa hali ya kusifiwa yule mwenye kuitoa na mara nyingine hali ya kusemwa vibaya yule mwenye kukataa kuitoa. Kwa mfano pale kuliposemwa:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah.” (73:20)

الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“… wale ambao wanaamini mambo yaliyofichikana na husimamisha swalah na hutoa sehemu katika vile tulivyowaruzuku…” (02:03)

وَوَيْلٌ لِّلْمُشْرِكِينَ الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ

“Na ole kwa washirikina. Ambao hawatoi zakaah nao ni wenye kuikanusha Aakhirah.” (41:6-7)

Dhahiri ya zakaah hizi ni zile swadaqah zilizofaradhishwa pasi na kuanishwa vidhibiti na viwango vyake. Hayo yaliyowekwa katika Shari´ah Madiynah – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 14-17
  • Imechapishwa: 12/05/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy