44. Tafiti kuhusu kusihi kwa ile twahara pindi unapomalizika muda wa kupangusa au akavua kile kitu kinachofunika mguu

Tafiti ya tano inahusu kusihi kwa ile twahara pindi unapomalizika muda wa kupangusa au akavua kile kitu kinachofunika mguu.

Wanazuoni wametofautiana juu ya hilo. Imekuja katika “al-Majmuu´”[1].

Maoni ya kwanza yanasema kuwa twahara ni yenye kubaki na hakuna kitu kinachomlazimu mtu. Kwa hivyo ataswali kwa twahara yake muda wa kuwa hajapatwa na hadathi. Ibn-ul-Mundhir amesema kuwa hayo ndio maoni alionayo al-Hasan al-Baswriy, Qataadah, Sulaymaan bin Harb na yeye mwenyewe akayachagua. an-Nawawiy amesema:

“Ndio maoni yaliyochaguliwa na yenye nguvu.”

Vilevile ndio maoni yaliyochaguliwa na Ibn Hazm[2]. Inapokuja katika suala la muda wa kupangusa, amesema kuwa maoni alionayo Ibraahiym an-Nakha´iy, al-Hasan al-Baswriy, Ibn Abiy Laylaa na Daawuud. Kisha akasema:

“Haya ndio maoni pekee yanayojuzu.”

Ibn Hazm amesema tena:

“Akipangusa dakika moja kabla ya kumalizika kwa muda, basi inafaa kwake kuswali kwa hali hiyo midhali wudhuu´ wake haujachenguka.”[3]

Na kuhusu kwamba wudhuu´ wake hauchenguki pindi anapovua kile kitu kinachofunika mguu, amesema:

“Hayo ni maoni ya kikosi katika Salaf.”[4]

Maoni yote mawili yamechaguliwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

Maoni ya pili yanasema kuwa mtu analazimika kuosha miguu peke yake. Hayo ndio maoni alionayo ´Atwaa’, ´Alqamah na al-Aswad. Amenukuu maoni hayohayo kutoka kwa an-Nakha´iy. Pia ndio maoni ya Abu Haniyfah na wenzake, ath-Thawriy, Abu Thawr, al-Muzaniy na moja ya upokezi kutoka kwa Ahmad.

Maoni ya tatu yanasema kuwa ni lazima kwa mtu huyo kutawadha. Hivo ndivo alivoonelea Mak-huul, an-Nakha´iy, az-Zuhriy, Ibn Abiy Laylaa, al-Awzaa´iy, al-Hasan bin Swaalih, Ishaaq na ndio moja ya upokezi sahihi zaidi kutoka kwa Ahmad.

Maoni ya nne yanasema kuwa analazimika kutawadha ukirefuka sana muda kuanzia pale atapovua kile kitu kinachofunika mguu mpaka pale atakapoosha miguu. Vinginevyo itatosha kuosha miguu. Haya ndio maoni alionayo Maalik na al-Layth.

Mpaka hapa yamekamilika yale niliyotaka kuandika. Namwomba Allaah (Ta´ala) anufaishe kwayo. Kwani hakika yeye ni Mwingi wa kutoa na mkarimu. Yameandikwa siku ya 16 Rabiy´ ath-Thaaniy 1407.

[1] ”al-Majmuu´” (1/511).

[2] Tazama ”al-Muhallaa” (2/94).

[3] al-Muhallaa (2/95).

[4] al-Muhallaa (2/105).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/188-189)
  • Imechapishwa: 11/05/2021