43. Tafiti kuhusu pindi inapobadilika ile hali ya upangusaji kutoka katika hali ya ukazi kwenda katika hali ya safari au kinyume chake

Tafiti ya nne inahusu pindi inapobadilika ile hali ya upangusaji kutoka katika hali ya ukazi kwenda katika hali ya safari au kinyume chake.

Sura hii ina hali tatu:

Ya kwanza: Hali ikabadilika kabla ya kuchenguka kwa wudhuu´. Kwa mfano amevaa soksi za ngozi akiwa ni mkazi kisha akaanza safari yake kabla ya kuchengukwa na wudhuu´ au akazivaa akiwa msafiri halafu akafika katika mji wake kabla ya wudhuu´ wake kuchenguka.

Katika mfano wa kwanza anatakiwa kufuta kama vile msafiri. Katika “al-Majmuu´” imetajwa kwamba kuna maafikiano juu ya hilo[1].

Katika mfano wa pili atatakiwa kupangusa kama mkazi. Hakuna utatizi juu ya hilo.

Ya pili: Hali ikabadilika baada ya kuchengukwa na wudhuu´ na kabla ya kupangusa. Mfano wa hilo mtu akavaa soksi za ngozi katika mji wake, kisha akachengukwa na wudhuu´ halafu akaanza safari kabla ya kupangusa au akazivaa akiwa ni msafiri, wudhuu´ wake ukachenguka kisha akafika katika mji wake kabla hajapangusa.

Katika mfano wa kwanza anatakiwa kupangusa kama msafiri. Imekuja katika “al-Inswaaf”:

“Hivi ndivo yanavosema madhehebu na ndio maoni ya wenzetu.”[2]

Katika “al-Furuu´” ameambatanisha herufi و akiashiria kwamba maimamu watatu wameafikiana kwa maoni hayo[3]. Kisha akasema:

“Ahmad pia ana maoni yanayosema kuwa anatakiwa kupangusa kama mkazi.”

Imekuja katika “al-Mughniy”:

“Ambaye bado hajapangusa kisha akaanza kusafiri anatakiwa kufuta kama msafiri. Hatujui tofauti yoyote kutoka kwa wanazuoni juu ya hilo.”[4]

Katika mfano wa pili anatakiwa kupangusa kama msafiri. Sijaona tofauti yoyote juu ya hilo.

Ya tatu: Hali ikabadilika baada ya kuchengukwa na wudhuu´ na kupangusa. Kwa mfano mtu akavaa soksi za ngozi katika mji wake, akazipangusa kisha akasafiri au akavaa soksi za ngozi katika safari, akazipangusa kisha akafika katika mji wake. Wanazuoni wametofautiana katika hali kama hii.

Kuhusiana na mfano wa kwanza, ima iwe ule muda wa kupangusa wa mkazi umemalizika au bado unaendelea. Ikiwa umemalizika, basi haifai kwake kuzipangusa. Sijaona tofauti yoyote juu ya hilo isipokuwa yale yaliyosemwa na Ibn Hazm katika “al-Muhallaa” kwamba anatakiwa kukamilisha upangusa akiwa kama msafiri[5].

Na ikiwa ule muda wa kupangusa bado unaendelea, wanazuoni wametofautiana juu ya hilo. Madhehebu ya Maalik, madhehebu ya ash-Shaafi´iy, moja ya maoni ya Ahmad, Ishaaq na moja ya maoni ya Daawuud yanasema kuwa anatakiwa kupangusa kama mkazi. Madhehebu ya Abu Haniyfah na ath-Thawriy wanaona kuwa anatakiwa kupangusa kama msafiri. Vilevile ni moja ya maoni ya Ahmad na ya Daawuud[6].

Imekuja katika “al-Mughniy”:

“al-Khallaal amesema: “Ahmad amejirejea katika yale maoni yake ya mwanzo na akaja katika maoni haya.”[7]

Imekuja katika “al-Inswaaf” kwamba mtunzi wa “al-Faaiq” amesema:

“Ndio maoni ya nyuma na ndio yenye kuchaguliwa.”[8]

Kuhusu mfano wa pili, ima iwe ule muda wa kupangusa wa msafiri umemalizika au bado unaendelea. Ikiwa umemalizika, basi haitofaa kwake kupangusa.”

Na ikiwa ule muda wa kupangusa bado unaendelea, basi atapangusa kama mkazi. Imekuja katika “al-Mughniy”:

“Haya ndio maoni ya ash-Shaafi´iy na Hanafiyyah. Simjui mwingine ambaye ameonelea kinyume.”[9]

Katika “al-Furuu´” ameambatanisha herufi و akiashiria kwamba maimamu watatu wameafikiana kwa maoni hayo[10]. Kisha akasema:

“Katika “al-Mabhaj” imekuja: “Anatakiwa kupangusa kama msafiri ikiwa amefanya hivo zaidi ya mchana mmoja na usiku wake.”

Imekuja katika “al-Muhallaa”:

“Anatakiwa kuanza kupangusa kama mkazi akiwa amekwishapangusa safarini kipindi kisichopongua michana miwili na nyusiku mbili. Lakini ikiwa bado umebaki ule muda wa kupangusa basi atapangusa kama msafiri.”[11]

[1] al-Majmuu´ (1/472).

[2] al-Inswaf (1/179).

[3] al-Furuu´ (1/168).

[4] al-Mughniy (1/290).

[5] al-Muhallaa (2/109).

[6] Tazama “al-Majmuu´” (1/472).

[7] al-Mughniy (1/292).

[8] al-Inswaaf (1/178).

[9] al-Mughniy (1/293).

[10] al-Furuu´ (1/168).

[11] al-Muhallaa (2/109).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/186-188)
  • Imechapishwa: 11/05/2021