Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Vita ni vyenye kuendelea pamoja na viongozi wema na waovu mpaka siku ya Qiyaamah na haitakiwi kuachwa. Kiongozi kugawa fai na kusimamisha adhabu ni mambo yenye kuendelea. Hakuna yeyote aliye na haki ya kuwaponda wala kupambana nao. Inafaa na ni sahihi kuwapa zakaah sawa wakiwa wema au waovu.

MAELEZO

Utambuzi na hukumu ya jihaad ni yenye kubaki, lakini pale yanapotimia masharti yake na vikaondoka vikwazo. Jihaad ni katika faradhi na matendo bora ya Uislamu kwa sababu yanapelekea ushindi wa dini na kuinyanyua haki juu. Lakini haijuzu kujiweka khatarini. Ni lazima jambo liangaliwe vyema ili masharti ya jihaad yawe yametimia na viondoke vikwazo vyake ili nchi ya Kiislamu iweze kupambana. Wakati mtawala wa Kiislamu atapomua kumshambulia adui wa Allaah basi ataanza kuwalingania. Wakikataa hapo jihaad itakuwa imewekwa katika Shari´ah.

Ni lazima kwa kila ambaye anaitwa na kiongozi kuitikia ulingano na ajiunge na jeshi la waislamu. Wanapaswa kumtii mtawala ni mamoja ni mwema au muovu. Mtawala anaweza kuwa muovu kwa maana ya kwamba anatenda madhambi makubwa, lakini muda wa kuwa ni muislamu raia wake wanapaswa kumwitikia pale anapowaita kujiunga na jeshi lake. Bali wanalazimika kutekeleza amri yake katika yaliyo mema, kupambana chini ya uongozi wake na kuswali nyuma yake ikiwa yeye ndiye imamu. Haijuzu kwako kumuasi kabisa.

Huu ndio msimamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya viongozi hata kama watakuwa madhalimu. Jambo ni baya zaidi ikiwa ni wema; wana haki zaidi ya kutiiwa na kushirikiana nao katika yaliyo mema na utiifu, khaswa mtawala anayekuamrisha kuinusuru ´Aqiydah, mfumo wa Uislamu wa kimatendo na kueneza haki inayopelekea kupata maisha mazuri duniani na Aakhirah. Tunamshukuru Allaah ambaye ametuokoa kutokana na fikira za Khawaarij waliochupa mipaka na Raafidhwah wapotevu na waliopinda.

Fai ni zile ngawira za vita ambazo Allaah anawaruhusu waislamu kuzinyakua kutoka kwa makafiri kwa sababu ya kupambana jihaad katika njia ya Allaah na kuwashinda maadui zao. Baada ya hayo, ni lazima kwa mtawala au naibu wake aweke kando 1/5 ngawira za vita na kuwapa wale wapambanaji 4/5. Hadiyth inasema kwamba mpanda farasi anapaswa kupata mafungu mawili ya askari anayetembea kwa miguu.

Si haki ya kila mmoja kusimamisha adhabu za Kishari´ah. Isipokuwa yule aliyetawalia madaraka ya waislamu. Mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye haki ya kusimamisha adhabu kama vile ya kumuua anayeua makusudi, anakata mkono wa mwizi, anampiga bakora mzinzi ambaye hajawahi kuingia ndani ya ndoa, atampiga mawe mzinzi ambaye kishawahi kuingia ndani ya ndoa na atampiga mijeledi mtu ambaye anawatuhumu wengine machafu na mnywaji pombe. Wakati mwingine adhabu inaweza kuwa kwa njia ya kuua. Yote haya ni mambo yanayopasa mamlaka. Hakuna mwengine yeyote, hata kama ni mwanachuoni,  anayo haki ya kusimamisha adhabu si juu ya nafsi yake mwenyewe wala waja wengine isipokuwa ikiwa kama ana idhini kutoka kwa mtawala, kwa mfano mahakimu wa kidini na maafisa wa polisi. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya jambo hili.

Hakuna yeyote mwenye haki ya kuwatukana, kuwatia aibu na kuwakashifu watawala. Matendo hayo yanapelekea katika vurugu na shari. Hakuna mtu yeyote, haijalishi kitu ni ubora gani alionao, anayo haki ya kuvutana nao juu ya utawala wao. Kwa maana ya kwamba ikiwa kuna mtawala anayekubalika kwa mujibu wa Shari´ah na kukawepo mwengine ambaye ni mbora zaidi, haifai kwa yeyote kufuta serikali ya yule wa kwanza kwa sababu ya ubora wa huyu wa pili. Kwa sababu mambo hayo yanapelekea kumwagika kwa damu, kukiuka heshima za watu na kuporwa kwa mali za watu. Kwa msemo mwingine ni lazima kuwaheshimu watawala wote. Allaah huwalinda waislamu na miundombinu kupitia watawala. Adhabu za Kishari´ah na nembo za Kiislamu zinatekelezwa kupitia watawala. Watu wanahisi amani na wanaweza kusoma, kufanya biashara na mambo mengine ya kidini na ya kidunia. Mahali kokote anakosekana mtawala basi hutokosa uporaji na machafuko, nembo za kidini hazisimamishwi, misikiti na duara za kielimu zinasuswa na kila mmoja anashika silaha mkononi. Kutokana na fadhilah za Allaah watu wanaweza kuhisi amani chini ya mamlaka ya mtawala wa Kiislamu.

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 116-118
  • Imechapishwa: 14/05/2026