44. Radd ya pili juu ya makafiri wenye kupinga kufufuliwa

Vivyo hivyo Allaah (Jalla wa ´Alaa) ametumia hoja kwamba anaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Utaiona ardhi kame isiyokuwa na kitu; hakuna kijiti wala ujani. Allaah akateremsha juu yake mvua. Kisha ikaanza kutoa mimea na baada ya kipindi fulani kila mahali kukaenea kijani kibichi kwa aina mbalimbali ya mimea, maua na matunda ilihali hapo kabla ilikuwa ni kame. Ni nani ambaye ameirudisha kuwa hivi na kuihuisha? Ambaye ni muweza wa kuhuisha ardhi ni muweza wa kuihuisha miili:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

”Miongoni mwa alama Zake ni kwamba utaona ardhi imetulia kame, kisha tunapoiteremshia maji inatikisika na huotesha. Hakika Yule aliyeihuisha, bila shaka ni Mwenye kuhuisha wafu, hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.”[1]

Ambaye anaihuisha ardhi baada ya kufa kwake ni muweza wa kuwahuisha wafu baada ya kufa kwao na kuwarudisha kama walivyokuwa. Hii ni miongoni mwa dalili juu ya kufufuliwa; kuihuisha ardhi kwa mimea baada ya kufa kwake.

[1] 41:39

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 66
  • Imechapishwa: 06/04/2021