44. Kuyatembelea makaburi kunatakiwa kumnufaishe aliye hai na maiti

Imependekezwa kuyatembelea makaburi. Yanawakumbusha waliohai Aakhirah na yanawafurahisha wale maiti pindi waliohai wanapowasomea Qur-aan, kuwaombea msamaha, kuwaombea du´aa, kuwatolea swadaqah na kadhalika. Kuyatembelea makaburi kuna manufaa kwa waliohai na wale maiti. Kama tulivyosema aliye hai anakumbuka Aakhirah na mauti. Pindi anakumbuka kile kidogo kilicho Aakhirah, basi anakiona kikubwa. Anapokumbuka vingi vilivyoko duniani, anavidharau. Asome Aayah za kuhusu subira na kwamba dunia hii karibu itatoweka:

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ

“Je, haujafika wakati kwa walioamini zinyenyekee nyoyo zao kwa ukumbusho wa Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawarefukia muda, halafu zikawa ngumu nyoyo zao – na wengi miongoni mwao wakatumbukia katika madhambi na kuasi?” 57:16

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ

“Je, mlidhania kuwa Sisi tulikuumbeni kwa ajili ya mchezo na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” 23:115

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alishika kwenye mabega na kunambia: “Ishi duniani kama mgeni au mpita njia.”

Ibn ´Umar alikuwa akisema:

“Ukifikisha jioni usitarajii kuwa utafikisha asubuhi. Ukifikisha asubuhi usitarajii kuwa utafikisha jioni. Chukua kutoka katika siha yako uyape maradhi yako na uchukue kutoka katika maisha yako uyape mauti yako.”

Akiyafikiria hayo atakuwa na unyenyekevu na kuacha kufanya madhambi. Vilevile atawakumbuka ndugu na wapendwa waliotangulia. Haya ndio matembezi yenye manufaa na sio kama watu wajinga wa leo wanavyofanya kwa matembezi yao ya Bid´ah ya siku ya alhamisi na jumamosi na wanawake kujipamba na kwenda na kuyakalia makaburi. Abu Daawuud amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu kukaa juu ya kaa likaunguza nguo zake na likaingia mpaka kwenye ngozi yake ni bora kwake kuliko kukaa juu ya kaburi.” Muslim (971).

Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msikae juu ya makaburi na wala msiswali kuyaelekea.”

Hata hivyo wanachuoni wametofautiana kipi kinachomaanishwa na kukaa juu ya kaburi. Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa maana yake ni ukaaji wa kawaida unaojulikana. Maalik amesema kuwa maana yake ni kufanya haja juu yake. Amepokea katika “al-Muwattwa” yake ya kwamba ´Aliy alikuwa akiyaegemea makaburi, kwamba Ibn ´Umar alikuwa akikaa juu ya makaburi na kwamba ´Uthmaan bin Hukaym amesema:

“Khaarijah bin Zayd alinishika mkono na kunambia nikae juu ya kaburi na kunambia kuwa ami yake Zayd bin Thaabit amesema: “Kilichochukizwa ni kufanya haja juu yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 14/10/2016