45. Yaliyopendekezwa wakati wa kuyatembelea makaburi

Imaam Ahmad amesema:

“Makaburi yanatakiwa kutembelewa siku ya ijumaa kabla ya jua kuchomoza. Wale maiti wanawaona wale wanaowatembelea.”

al-Ghazaaliy amesema katika “Ihyaa´ ´Uluum-id-Diyn”:

“Matembezi yanatakiwa kuwa siku ya ijumaa na siku ya jumamosi kabla ya jua kuchomoza.”

Imependekezwa kuyakumbuka mauti sana. Imethibiti kwa at-Tirmidhiy aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kithirisheni kukumbuka kile kinachokata ladha.”

Bi maana kifo.

Pindi mtu anapoingia makaburini imependekezwa kuwatolea salamu wale waliyomo ndani ya makaburi. Muslim amepokea kupitia kwa Sulaymaan bin Buraydah aliyesimulia kuwa baba yake amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafunza kipi cha kusema wanapofika makaburini. Walikuwa wakisema:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين، وإنا إن شاءالله بكم لاحقون، نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waislamu na waumini. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.” Muslim (974).

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilimuomba idhini Mola wangu kumuombea msamaha mamangu, hakunipa ruhusa. Nikamuomba idhini ya kutembelea kaburi lake, akanipa ruhusa. Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanawakumbusheni Aakhirah.”

´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilikuwa nimekukatazeni kuyatembelea makaburi. Yatembeleeni! Kwani hakika yanawakumbusheni Aakhirah.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 93-95
  • Imechapishwa: 14/10/2016