43. Subira ya Salaf kwa kufiliwa na watoto wao

Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy ya kwamba Anas amesema:

“Mtoto wa kiume wa Abu Twalhah aliumwa. Akafariki pindi baba yake Abu Twalhah alipokuwa ametoka nje. Wakati mke wake alipoona kuwa ameshakufa akajiandaa kwa kiasi fulani na akamuweka mtoto yule upande mwingine wa nyumba. Pindi Abu Twalhah alipofika nyumbani akasema: “Mtoto anaendeleaje?” Akamwambia: “Ametulia. Natumai sasa yuwastarehe.” Abu Twalhah akafikiri kuwa anasema ukweli na akalala. Alipoamka asubuhi na kuoga na kutaka kutoka nje, akamweleza kuwa amefariki. Akaswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha akamweleza yaliyompitikia. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Huenda Allaah akawabariki katika usiku wao.” Mwanaume mmoja katika Answaar akasema: “Niliona jinsi walivyopata watoto kumi na wote walikuwa wamehifadhi Qur-aan.”

Upokezi mwingine unasema ya kwamba pindi mtoto wake alipokufa mwanamke yule aliwaambia familia yake: “Asiwepo yeyote atayezungumza na Abu Twalhah kabla yangu.” Alipoingia nyumbani akamuulizia mtoto. Akajibu: “Hajapatapo kutulia.” Akampa chakula akala. Kisha akajiandaa mpaka akamwingilia.

Mwanamke huyu alisubiri, akaridhia, akawa imara na akatarajia malipo kutoka kwa Allaah. Kwa ajili hiyo Allaah akampa kilicho bora kuliko kile kilichomsibu. Mtu akimtazama mwanamke aliyepatwa na msiba anayefanya vitu ambavyo vinafanywa na mtu tu ambaye yuko na furaha, mtu anapaswa kuiga na kujifunza sifa za wahenga waliotangulia. Vilevile wanaume wanatakiwa kujua kuwa wao ndio wana haki zaidi ya kufanya hivi na kusubiri kuliko wanawake.

Hakuna mwanamke aliyefikwa na msiba kama msiba uliyomfika Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ni bingwa wa wanawake wa Peponi. Alifikwa na msiba wa kufariki kwa baba yake, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika hali hii nzito hakusema jengine isipokuwa haki. Alisema:

“Baba mpendwa! Ukaribu uliyoje Mola wake yuko! Baba mpendwa! Tunamweleza Jibriyl kifo chake! Baba mpendwa! Ameitikia wito wa Mola wake! Baba mpendwa! Makazi yake ni Peponi!”

Linalotupasa ni kuwaiga wanaume na wanawake mabingwa.

Pindi mvulana wa mwanaume mmoja katika Salaf alipofariki Sufyaan bin ´Uyaynah, Muslim bin Khaalid na wengine wakampa pole. Alikuwa katika huzuni mkubwa mpaka al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw akaja na kumwambia: “Unaonaje lau wewe na mwanao mngekuwa mmefungwa gerezani na mwanao akatoka jela, usingefurahi?” Mwanaume yule akasema: “Ndio.” al-Fudhwayl akamwambia: “Mwanao ametoka kwenye gereza ya dunia hii kabla yako.” Mwanaume yule akafurahi na kusema: “Nimepewa pole.” Ameipokea Haafidhw Ibn ´Asaakir.

Maalik amesimulia kuwa amefikiwa ya kwamba Sa´iyd bin Yasaar amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini hatoacha kusibiwa kwa mtoto na wapenzi wake mpaka akutane na Allaah ilihali hana dhambi yoyote.”

Imeshatangulia yaliyopokea Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy kutoka katika Hadiyth ya Abu Muusa al-Ash´ariy. Kinacholengwa ni kwamba atayesikia Hadiyth hii baada ya kufikwa na msiba anapata maliwazo ndani yake.

Pindi Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) yalipomfikia mauti akaangusha kilio. Akaambiwa: “Kipi kinachokuliza?” Akasema: “Nalia kwa sababu safari ni ndefu na zawadi ni ndogo. Yakini ni dhaifu na mbele yangu nina kizingiti ambapo ima ni kuingia Peponi au Motoni.”

Pindi ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz yalipomfika mauti akasema: “Nikazeni.” Wakamkaza na akasema: “Ee Allaah! Mimi ndiye ambaye umeniamrisha nikafanya mapungufu. Ukanikataza nikaasi. Ukinisamehe umenineemesha. Ukiniadhibu hukunidhulumu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe.”

Sulaymaan at-Taymiy amesema:

“Niliingia kwa rafiki yetu mmoja ambaye alikuwa amekaa akihuzunika. Nikahisi vibaya kwa niliyoyaona. Nikamwambia: “Huzuni wote huu ni wa nini ilihali ulikuwa katika hali njema?” Akasema: “Kwa nini nisihuzunike? Ni nani anatakiwa kuhuzunika sana zaidi yangu? Ninaapa kwa Allaah lau Allaah atanisamehe basi ningelikuwa na haya kutokana na yale yote niliyomfanyia.”

Pindi ´Abdul-Malik bin Marwan yalipomfika mauti alisema:

“Ninaapa kwa Allaah natamani ningelikuwa mtumwa mwenye kuchunga kondoo mlimani kutoka katika Tihaamah kuliko kuwa mfalme.”

al-Muzaniy amesema:

“Niliingia kwa ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) pindi alipokuwa na maradhi aliyokufa kwayo. Nikamuuliza anavyoendelea. Akasema: “Nakaribia kuiaga dunia. Nakaribia kutengana na ndugu zangu. Nakaribia kukutana na matendo yangu maovu. Nakaribia kunywa kikombe cha kifo. Nakaribia kukutana na Allaah (´Azza wa Jall). Ninaapa kwa Allaah sijui kama nitaingia Peponi, ili nijipe hongera mwenyewe, au Motoni, ili nijiliwaze mwenyewe?” Kisha akaanza kulia.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 85-88
  • Imechapishwa: 14/10/2016