43. Ulazima wa kulipa siku zilizompita mtu Ramadhaan

Kila ambaye imefaa kwake kuacha kufunga kutokana na moja ya sababu zilizotangulia basi hakemewi kwa kula kwake hadharani waziwazi ikiwa sababu yake ni yenye kuonekana kama mfano wa mgonjwa na mzee asiyeweza kufunga. Lakini sababu ya kutokufunga kwake ikiwa ni yenye kujificha, kama mfano wa mwenye hedhi na mwenye kumwokoa kifo aliyelindwa kuuliwa, basi ale kwa kujificha na wala asionyeshe waziwazi kula kwake ili asijisababishie tuhuma juu ya nafsi yake na ili mjinga asidanganyike na akafikiri kuwa inafaa kuacha kufunga bila ya udhuru wowote.

Kila ambaye amelazimika kulipa kutokana na yale mafungu yaliyotangulia basi atalipa kwa idadi ya siku alizoacha kufunga. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“… hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Akila mwezi mzima basi atalazimika kulipa mwezi mzima. Ikiwa mwezi umeishilia siku thelathini basi atalazimika kulipa siku thelathini. Ikiwa mwezi umeishilia siku ishirini na tisa basi atalazimika kulipa siku ishirini na tisa peke yake.

Bora ni kuharakisha kulipa pale tu ambapo udhuru utaondoka. Kwani kufanya hivo ni kuiharakia zaidi kheri na kuitakasa dhimma yake.

Inafaa pia kuchelewesha mpaka pale ambapo kutabaki kati yake yeye na Ramadhaan inayofuata kwa kiasi cha siku anazodaiwa. Amesema (Ta´ala):

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

” Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni magumu.”

Miongoni mwa utimilifu wa wepesi ni kuchelewesha kulipa. Ikiwa anadaiwa siku kumi za Ramadhaan basi itafaa kuchelewesha mpaka pale ambapo hakutobaki kati yake yeye na Ramadhaan ya pili isipokuwa tu siku kumi.

Haijuzu kuchelewesha kulipa deni mpaka ikaingia Ramadhaan ya pili pasi na kuwa na udhuru. Hilo ni kutokana na maneno ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Nilikuwa na deni la Ramadhaan na siwezi kulilipa isipokuwa katika Sha´baan.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Jengine ni kwa sababu kuchelewesha mpaka ikaingia Ramadhaan ya pili kunapelekea kukusanyikiwa na swawm na pengine zikamshinda au akafa. Isitoshe swawm ni ´ibaadah yenye kujikariri. Kwa hiyo haitofaa kuchelewesha ile ya kwanza mpaka ikaingia ya pili kama ilivyo swalah.

Udhuru ukiendelea juu yake mpaka akafa basi hana dhambi juu yake. Kwa sababu Allaah amemuwajibishia kutimiza katika masiku mengineyo. Lakini ikiwa hakuweza na hivyo imedondoka kwake kama ambaye amekufa kabla ya kuingiliwa na mwezi wa Ramadhaan. Mtu huyo hatolazimika kulipa. Akiweza kulipa deni lake lakini hata hivo akazembea juu yake hadi akafa, basi ndugu yake atamfungia masiku yote ambayo alikuwa na uwezo wa kuyafunga. Hayo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kufa na anadaiwa swawm basi atafungiwa na walii wake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Walii wake ni yule mwenye kumrithi au ndugu yake.

Inafaa akafungiwa na jopo la watu kwa idadi ya siku anazodaiwa kwa muda wa siku moja. al-Bukhaariy amesema, al-Hasan amesema:

“Itafaa kufungiwa na watu thelathini siku moja.”

Asipokuwa na walii au akawa na walii asiyetaka kufunga basi atatolewa chakula kutoka katika mirathi yake kumpa maskini kwa kila siku moja kwa idadi ya siku alikuwa na uwezo wa kulipa. Kila maskini atapewa Mudd ya ngano nzuri ambayo ni sawa na nusu kilo na gramu kumi.

[1] 02:184

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 11/05/2020