43. Siku ambayo kila mmoja atalipwa kwa alichokifanya

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ

”Mfalme wa siku ya Malipo!”[1]

Ni siku ya malipo na hesabu. Siku ambayo kila mmoja atalipwa kwa matendo yake. Kama ni mema malipo yatakuwa mema, na kama ni shari malipo yatakuwa shari. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”[2]

Hadiyth kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye akili ni yule ambaye anaibidisha nafsi yake na kufanyia kazi kwa yanayomgonja baada ya mauti na asiye muweza ni yule ambaye anafuata matamanio ya nafsi yake na huku akiwa na matumaini ya uongo kwa Allaah.”[3]

MAELEZO

Ni siku ya malipo na hesabu. Amefasiri الدِّينِ kwa maana ya malipo na hesabu. Neno الدِّينِ huja likiwa na maana nyingi. Linaweza kuwa na maana ya malipo, kama ilivyo katika Aayah hii. Vilevile linaweza kuwa na maana ya ´ibaadah. Amesema (Ta´ala):

وَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Mwombeni Yeye hali ya kumtakasia Yeye dini.”[4]

Bi maana kwa kumtakasia Yeye ´ibaadah.

مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ

”Mfalme wa siku ya Malipo!”

Ni siku ya Qiyaamah. Imeitwa siku ya Malipo kwa sababu watalipwa na kufanyiwa hesabu viumbe juu ya matendo yao. Kwa ajili hiyo mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) akasema:

”Siku ambayo kila mmoja atalipwa kwa matendo yake. Kama ni mema malipo yatakuwa mema, na kama ni shari malipo yatakuwa shari.”

Yule ambaye atafanya kheri basi atalipwa kheri na yule ambaye atafanya shari atalipwa shari. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ataiona.”[5]

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo? Kisha nini kitakachokujulisha siku ya malipo? Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”

Dalili ya kwamba kila mmoja atalipwa kwa matendo yake. Ametukuza (Subhaanah) siku hiyo na akasema:

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ

”Ni kipi kitakachokujulisha siku ya malipo?”

Akakariri kuitukuza kutokana na ukubwa wake na kutukuza na jambo lake. Kisha akafasiri na kusema:

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِّنَفْسٍ شَيْئًاۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”Siku ambayo nafsi haitomiliki chochote juu ya nafsi nyingine na amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”

Hapa nafsi kunaingia nafsi zote ikiwemo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ndio nafsi bora. Haitomiliki kwa ajili ya mwengine chochote. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati Allaah (´Azza wa Jall) alipomteremshia:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Na waonye jamaa zako wa karibu.”[6]

akasema:

“Enyi Quraysh – au maneno mfano wa haya – Zinunueni nafsi zenu! Hakika sintokufaeni mbele ya Allaah na chochote. Ee ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib! Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote! Ee Swafiyyah, shangazi yake Mtume wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote. Ee Faatwimah, binti ya Muhammad! Niombe chochote katika mali yangu utakacho. Sitokufaa mbele ya Allaah na chochote.”[7]

وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ

”… amri siku hiyo ni ya Allaah pekee.”

pekee yake. Hakuna yeyote yule ambaye atamiliki chochote. Viumbe wote watakuwa kimya na Allaah atawafanyia hesabu na kuwalipa.

[1] 01:03

[2] 82:17-19

[3] at-Tirmidhiy (2459) aliyesema ni nzuri, Ibn Maajah (4260) na Ahmad (17123). at-Tirmdhiy amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri.”

al-Haakim  amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti ya al-Bukhaariy japo hakuipokea.” (al-Mustadrak (01/125)).

[4] 07:29

[5] 99:07-08

[6] 26:214

[7] al-Bukhaariy (2753) na Muslim (204).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 72-73
  • Imechapishwa: 16/06/2022