43. Mtume aliyekuwa akijitengenezea mkate wake

249 – Ameeleza pia kwamba amemsikia akisema:

”Siku moja rafiki yangu mmoja aliniita kuja kula, tumbo langu likanambia: ”Niondoshee matamanio yako mara hii.” Ikafanya hivo. Akaniita mara nyingine, ambapo nafsi yangu ikaniomba kumwendea. Nikaimbia: ”Ifanye mara hii iwe kama mara ya kwanza; je, ungehisi ladha yoyote endapo ungelikuwa umefanya?” Sikuacha kutoa sababu mpaka ikatulizana. Kisha baada ya hapo nikaitwa na ndugu yangu mwingine tena, ambapo ikasema: ”Huyu ni ndugu yako na anazo haki mbili: haki ya udugu na haki ya kuitikia mwaliko. Mwendee. Hakika huyo yuko karibu zaidi na Allaah na kutadumisha udugu wenu.” Nikasema: ”Ole wako! Hebu acha kuwa mkarimu ili uweze kufikia yale unayoyapenda. Naapa kwa Allaah! Siku ya Qiyaamah utafurahi kwa uchache wa chakula na kuacha matamanio.” Ikakataa na kuwa mkorofi na kusema: ”Ukiendelea namna hiyo basi utaniua. Hebu nanyuka na wende kwa nduguyo!” Nikasimama. Naapa kwa Allaah! Nikahisi ni kana kwamba naburutwa usoni mwangu. Nikafika kwenye mwaliko baada ya kuwa wameshamaliza kula. Mwenyeji akasema: ”Kaa chini, Allaah akurehemu!” Akasimama kwa ajili ya kunihangaikia. Nikamwambia: ”Kaa chini! Naapa kwa Allaah hii leo hapa sintokula kitu.” Nikawaombea mema na nikasimama. Baada ya kuwa tumeshatoka nje, nikaiambia: ”Allaah amekudhalilisha. Hmdi zote ni za Allaah ambaye hakutimiza kile ulichokuwa unakitaka.” Ikasema: ”Ni kweli, naapa kwa Allaah. Ulipokaa chini na kufikiria, watu walikula na kuondoka zao.” Nikasema: ”Ole wako! Na vinginevyo ni vipi atakuwa muumini kama sio mwenye kufikiria, mwenye khofu, mwenye kujihadhari na adui zake, kutokana nawe na adui zako? Ee mwanadamu! Hata adui aliyekufa hawezi kukufanyia yale ambayo nafsi inaweza kukufanyia. ”

250 – Muhammad amesema: as-Swalt bin Hakiym ametuhadithia: Abu Ja´far al-Mukhawwaliy amesema:

”Moyo wenye njaa uko karibu na Allaah (´Azza wa Jall) na iko mbali zaidi na shaytwaan, karibu na kheri mbali na shari, karibu na mema mbali na maovu, karibu na urafiki mbali na maradhi.” Nikasema: ”Nini maana ya karibu na urafiki na mbali na maradhi?” Akasema: ”Anapopita karibu na vikao vya dhikr, anahisi urafiki na watu wake na akaketi nao. Na anapopita kwenye vikao viovu, nayo ndio maradhi yenyewe, anawakimbia.”

251 – Muhammad bin ´Abdillaah al-Madaniy ametuhadithia: Mu´tamar bin Sulaymaan ametuhadithia, kutoka kwa Abu Ka´b al-Hariyriy, ambaye amesema:

”Katika jiko la Daawuud (´alayhis-Salaam) kulikuwa kunatengenezwa mikate sabini ya ngano, ilihali yeye mwenyewe anakula mkate wa shayiri wa majani ya mitende, aliyotengeneza mwenyewe kwa mikono yake.”

252 – Haaruun bin ´Abdillaah ametuhadithia: Ma´n bin ´Iysaa ametuhadithia, kutoka kwa Mu´aawiyah bin Swaalih, kutoka kwa Abuz-Zaahiriyyah, ambaye amesema:

”Daawuud (´alayhis-Salaam) alikuwa akitengeneza vikapu, akaviuza na akila kutokana na chumo lake.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 151-154
  • Imechapishwa: 01/08/2023