43. Je, ni sharti katika kuswalisha mtu anuie uimamu?

Swali 43: Je, ni sharti katika kuswalisha mtu anuie uimamu? Mtu akiingia akamkuta mtu mwingine anaswali aongozwe naye? Je, imesuniwa kuswalishwa na mtu ambaye amekuja kuchelewa?

Jibu: Ni sharti kuweka nia ya kuswalisha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si venginevyo kila kitendo kinategemea nia na kila mmoja atalipwa kutokana na alivyonuia.”

Mtu akiingia msikitini na imeshampita swalah ya mkusanyiko akamkuta mtu anaswali peke yake basi hapana vibaya akaswali pamoja naye hali ya kuwa maamuma. Bali kufanya hivo ndio bora. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema baada ya kumuona mtu mmoja ameingia msikitini baada ya watu kumaliza kuswali:

“Hakuna mtu ambaye atamfanyia wema ambapo akaswali pamoja naye?”

Kwa kufanya hivo kunapatikana ubora wa swalah ya mkusanyiko kwa wote wawili. Ambaye amekwishaswali juu yake itakuwa ni swalah iliyopendekezwa.

Mu´aadh alikuwa akiswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya ´Ishaa ambayo ni faradhi kisha akirudi kwa watu wake na akiwaswalisha swalah hiyohiyo. Kwake yeye inakuwa ni swalah iliyopendekezwa na kwao inakuwa ni faradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkubalia jambo hilo.

Kuhusu ambaye amepitwa na sehemu ya swalah hapana neno akaswali nyuma yake ambaye imempita swalah ya mkusanyiko. Atapokamilisha swalah yule ambaye amepitwa na sehemu ya swalah basi atasimama kukamilisha yule ambaye hajakamilisha swalah yake kutokana na kuenea kwa dalili. Hukumu hii ni yenye kuenea juu ya swalah zote tano. Hilo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomtajia watawala watakaokuja ambao watachelewesha swalah nje ya wakati wake:

“Swali swalah ndani ya wakati wake. Utakapowawahi basi swali pamoja nao. Kwako itakuwa ni swalah iliyopendekezwa na wala usiseme “nimeshaswali na hivyo siswali tena.””

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 50-51
  • Imechapishwa: 30/08/2022