43. Je, anakufuru mtu ambaye anawapambia watu machafu na maovu?

Swali 43: Je, anakufuru mtu ambaye anawapambia watu machafu na maovu?

Jibu: Wale wanaolingania katika kufuru wanakufuru. Ama ikiwa wanawaita watu katika maasi yasiyokuwa kufuru na shirki hawakufuru[1]. Lakini wanapata dhambi kwa kitendo hicho. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote anayelingania katika uongofu basi anapata ujira mfano wa yule mwenye kumfuata pasi na kupungua chochote katika ujira wao. Na yeyote anayelingania katika upotevu basi anapata dhambi mfano wa yule mwenye kumfuata pasi na kupungua chochote katika dhambi zao.”[2]

Allaah (Ta´ala) amesema:

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ

 “Ili wabebe mizigo [ya madhambi] yao kamili Siku ya Qiyaamah na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya elimu – Zindukeni! Uovu ulioje wanayoyabeba!”[3]

[1] Mtu mwenye kanda ”ash-Shabaab; As-ilah wa Mushkilaat” amesema:

”Kuna kundi la wasanii mmoja au wengi. Kanda zao zinasambazwa na baadhi ya vijana wabaya. Kanda hizo ziko katika upeo wa mwisho wa machafu na mabaya. Zinazungumzia madhambi, machafu na uzinzi. Wanajifakhari kwazo. Wanatamani lau watu wote watakuwa namna hiyo. Naweza kusema kwa utulivu kabisa kuwa mtu kama huyu angalau kwa uchache kabisa anayadharau maasi. Hapana shaka yoyote ya kwamba ambaye anadharua dhambi na khaswa inapokuwa ni dhambi kubwa ya kuwa ni kufuru. Inahusiana na kikosi cha wasanii wanaotambulika, mtu mmoja au zaidi, ambao baadhi ya vijana wanaeneza kanda zao. Ni kufanya biashara kwa maovu na ni kutangaza kupambana vita na Allaah (´Azza wa Jall) kwa ujasiri na majigambo pasi na kuwa na hayaa. Ni jambo linalomfanya mtu kukata kabisa ya kwamba watu hawa hawaamini kuwa Allaah (Ta´ala) ameyaharamisha madhambi hayo. Hapana shaka yoyote kuwa matendo ya watu kama hawa ni kuritadi nje ya Uislamu. Nayasema haya hali ya kuwa ni mwenye kustarehe na moyo wangu umetulia juu ya msimamo huo.”

Mtu anaweza kufanya maasi na akayafanya kimakosa. Mtu kama huyu hurejea kwa upesi na akatubu na akamuomba msamaha Allaah kutokana na kosa lake.

Wakati mwingine mtu anaweza kufanya dhambi kwa sababu ya matamanio, shaytwaan na nafsi inayoamrisha sana maovu. Sambamba na hilo huku anaamini kuwa ni haramu. Mtenda dhambi kama huyo hayafanyi isipokuwa ni kwa sababu anayadharau na kuyadogesha, vinginevyo asingeyafanya. Mtu kama huyu hakufuru.

Kuhusu mtenda dhambi ambaye anaonelea madhambi kama vile uzinzi, unywaji pombe na ulaji ribaa ni halali, huyu hapana shaka yoyote juu ya ukafiri wake. Swali langu kwa muhadhiri huyu: ni nani aliyesema kuwa kuidharau dhambi ni kufuru?

Kile ambacho tunamwabudu Allaah kwacho ni kwamba ni maasi ambayo mtu anapaswa kutubu na kujirejea kwayo. Pale ambapo ataona kuwa ni halali basi hapo ndipo atakufuru kwa kule kuhalalisha.

[2] Muslim (2674), Ahmad (2/397), Abu Daawuud (4609) na at-Tirmidhiy (2674) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] 16:25

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 129-130
  • Imechapishwa: 28/02/2024