Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kutaka kinga ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa watu.” (an-Naas 114 : 01)

MAELEZO

Isti´aadhah ni kutaka kinga kutokana na kitu kinachotahadhariwa na kumegawanyika aina mbalimbali:

1- Kumuomba Allaah (Ta´ala) kinga. Imefungamana na ukamilifu wa kujidhalilisha Kwake, kutafuta nguvu Kwake na kuamini kutosheleza Kwake na kwamba Yeye ndiye mwenye kulinda kikamilifu na kila kitu. Ni mamoja kitu hicho ni cha hivi sasa au kinakuja huko mbele, kidogo au kikibwa, mtu au asiyekuwa mtu. Dalili Yake ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ مِن شَرِّ مَا خَلَقَ

“Najilinda na Mola wa mapambazuko, kutokamana na shari ya alivyoviumba.” (al-Falaq 113:01-02)

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ مَلِكِ النَّاسِ إِلَـٰهِ النَّاسِ مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ

“Najilinda na Mola wa watu, mfalme wa watu, mwabudiwa wa haki wa watu, kutokamana na shari za anayetia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma, anayetia wasiwasi nyoyoni mwa watu miongoni mwa majini na watu.” (an-Naas 114:01-05)

2- Kuomba kinga kwa sifa Zake kama maneno Yake, ukubwa Wake, utukufu Wake na mfano wa hayo. Dalili ya hayo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Najilinda kwa maneno ya Allaah yaliyotimia kutokamana na shari ya alichokiumba.”[1]

“Ee Allaah! Naomba kinga kwa utukufu Wako kuuliwa chini yangu.”[2]

Amesema katika du´aa ya maumivu:

“Najilinda kwa utukufu wa Allaah na uwezo Wake kutokamana na shari ninayohisi na kutahadhari nayo.”[3]

“Najilinda kwa radhi Zako kutokamana na hasira Zako.”[4]

Pindi kulipoteremka maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَن يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِّن فَوْقِكُمْ

“Sema: “Hakika Yeye ni muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu.” (al-An´aam 06 : 65)

akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Najilinda kwa uso Wako.”[5]

3- Kuwaomba kinga wafu au waliohai wasiokuweko mbele yako wasioweza kukulinda. Kitendo hichi ni shirki na miongoni mwa hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا

“Na kwamba walikuwa wanamme miongoni mwa watu wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia unyonge.” (al-Jinn 72 : 06)

4- Kuwaomba viumbe kinga kwa vitu wanavyoviweza. Kwa mfano ya watu, mahali na mfano wa hayo. Aina hii inafaa kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipokuwa anataja fitina:

“Mwenye kuielekea basi nayo itamwelekea, na mwenye kupata upenyo au kinga, ajikinge napo.”[6]

Kuna maafikiano juu yake.

Amebainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makimbilio na kinga hii pale aliposema:

“Yule ambaye yuko na ngamia basi aende naye.”[7]

Hadiyth ameipokea Muslim. Vilevile katika “as-Swahiyh” yake kuna Hadiyth ambayo imepokelewa na Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba kuna mwanamke mmoja kutoka katika kabila la Banuu Makhzuum ambaye aliiba. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoamrisha aletwe akaomba kinga kwa Ummu Salamah. Katika “as-Swahiyh” yake kwamba Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu atajilinda kwa Nyumba wakati atapotumiwa kikosi.”[8]

Endapo mtu ataomba ulinzi kutokamana na shari ya dhalimu, basi ni wajibu kumkinga kiasi cha mtu atakavyoweza. Hata hivyo ni haramu kumlinda iwapo anataka kufikia kitu kilichokatazwa au kukimbia kitu kimemuwajibikia.

[1] Muslim (2708), Abu Daawuud (3898), at-Tirmidhiy (2663), Ibn Maajah (3547), ad-Daarimiy (2680), Maalik (1832), Ahmad (6/377), Ibn Khuzaymah (2566) na Ibn Hibbaan (2689). Ibn Hajar ameiegemeza Hadiyth hii pia katika ”al-Mustakhraj” ya Abu ´Awaanah. Tazama ”Ittihaaf-ul-Maharah” (16/927).

[2] al-Bukhaariy katika ”at-Taariykh al-Kabiyr” (2278), Ahmad (2/25), Abu Daawuud (5074), an-Nasaa´iy (5544), Ibn Maajah (3871), al-Haakim (1/517) na Ibn Hibbaan (957). al-Haakim amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na haikupokelewa na al-Bukhaariy wala Muslim.”

adh-Dhahabiy amesema:

”Swahiyh.” (Talkhiys-ul-Mustadrak (1/517))

al-Albaaniy amesema:

”Swahiyh.” (at-Ta´liyqaat al-Hisaan (2/290))

[3] Muslim (2202), Ahmad (4/217), Abu Daawuud (3891), at-Tirmidhiy (2080), Ibn Maajah (2522) na Maalik (4/309) na al-Qabas.

[4] Muslim (222), Ahmad (1/96), Abu Daawuud (874), at-Tirmidhiy (3726), an-Nasaa´iy (1099), Ibn Maajah (3841) na at-Twahaawiy (1/234).

[5] al-Bukhaariy (7313), Ahmad (3/309), at-Tirmidhiy (3261), Ibn Hibbaan (7176) na Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (1/28).

[6] al-Bukhaariy (7082), Muslim (2886) na al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah” (68).

[7] Muslim (2887).

[8] Muslim (2882).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 64
  • Imechapishwa: 27/05/2020