Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kutaka msaada ni maneno Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.” (al-Faatihah 01 : 05)

Katika Hadiyth pia imekuja:

“Unapotaka msaada, basi mtake msaada Allaah.”

MAELEZO

Isti´aanah ni kutaka msaada na kumegawanyika sampuli mbalimbali:

1- Kumtaka msaada Allaah. Nako kumefungamana na mja kumdhalilikia Mola Wake kikamilifu, kuyagemeza mambo yake Kwake na kuamini kuwa anatosheleza. Hili hafanyiwi yeyote isipokuwa Allaah (Ta´ala). Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”

Uanisho huu umekuja katika neno “Wewe pekee” na kutokana na hilo inazingatiwa kuwa ni shirki kubwa inayomtoa mtu katika Uislamu akimfanyia mwengine asiyekuwa Allaah (Ta´ala).

2- Kumtaka msaada kiumbe kwa kitu anachokiweza. Hili linatokana na msaada wenye kuombwa; ikiwa ni jambo jema, basi inazingatiwa kuwa inajuzu kwa yule anayetakwa msaada na limesuniwa kwa yule mwenye kusaidia. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ

“Saidianeni katika wema na uchaji Allaah.” (al-Maaidah 05 : 02)

Ikiwa kitendo hicho kina madhambi, basi itakuwa ni haramu kwa yule mwenye kutaka na mwenye kutakwa msaada. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

”… na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” (al-Maaidah 05 : 02)

Ikiwa kitendo  ni chenye kuruhusiwa, basi inajuzu kwa yule mwenye kutaka msaada na mwenye kutakwa. Lakini hata hivyo yule mwenye kusaidia anaweza kulipwa thawabu kwa kitendo chake kizuri kumfanyia mwingine. Kwa ajili hiyo kitendo hicho kwa haki kinakuwa kimewekwa katika Shari´ah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

“Na fanyeni wema. Hakika Allaah anapenda watendao wema.” (al-Baqarah 02 : 195)

3- Kumtaka msaada kiumbe ambaye yuko hai na yuko mbele yako kwa kitu asichokiweza. Kitendo hichi ni upuuzi. Mfano wa kitendo kama hicho ni mtu kumtaka msaada mtu ambaye ni mdhaifu wa kubeba kitu kizito.

4- Kuwataka msaada wafu au kuwaomba viumbe wasiokuweko mbele yako na viumbe waliohai juu ya kitu kilichofichikana ambacho hawawezi kukifikia. Hili linazingatiwa kuwa ni shirki na linafanywa tu na mtu ambaye anaamini kuwa watu hawa wana uendeshaji wa kisiri juu ya ulimwengu.

5- Kutaka msaada kupitia matendo na hali zinazopendwa na Allaah (Ta´ala). Hichi ni kitendo kilichowekwa katika Shari´ah ambacho kimeamrishwa na Allaah (Ta´ala) pale aliposema:

اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ

“Tafuteni msaada kwa subira na swalah.” (al-Baqarah 02 : 153)

Kuhusu aina ya kwanza mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametumia dalili maneno Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”

Pia ametumia dalili kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Unapotaka msaada, basi mtake msaada Allaah.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 61
  • Imechapishwa: 27/05/2020