Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kutaka kuokolewa ni maneno Yake (Ta´ala):

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

“Na pindi mlipomuomba uokozi Mola wenu Naye akakujibuni.” (al-Anfaal 08 : 09)

MAELEZO

Istighaathah ni kule kutaka uokozi kutokamana na matatizo na maangamivu. Kumegawanyika aina mbalimbali:

1- Kumuomba uokozi Allaah (´Azza wa Jall), jambo ambalo ni katika matendo bora na kamilifu zaidi. Ni miongoni mwa sifa za Mitume na wafuasi wao. Dalili ya hilo ni yale aliyosema Shaykh (Rahimahu Allaah):

‘إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ

“Na pindi mlipomuomba uokozi Mola wenu Naye akakujibuni kuwa: “Hakika Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo.”

Hili lilikuwa katika vita vya Badr wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaangalia washirikina waliokuwa elfu wakati Maswahabah zake walikuwa juu kidogo ya mia tatu na ishirini. Akaingia ndani ya kibanda chake, akimlilia Mola Wake hali ya kuwa amenyanyua mikono akielekea Qiblah na huku akisema:

“Ee Allaah! Nitekelezee yale uliyoniahidi. Ee Allaah! Ukiangamiza kikosi hichi cha Kiislamu, basi hutoabudiwa tena katika ardhi.”

Ameipokea Muslim.

Hakuacha kumtaka uokozi Mola Wake hali ya kuwa amenyanyua mikono yake mpaka shuka yake ya juu ikaanguka kutoka kwenye mabegani mwake. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akaokota shuka yake ya juu na akairudisha mabegani mwake. Akakaa nyuma yake na kusema:

“Ee Mtume wa Allaah! Umemuomba Mola Wako vyakutosha. Hakika atakutekelezea yale aliyokuahidi.”[1]

Hapo ndipo Allaah aliteremsha Aayah hii.

2- Kuwaomba uokozi wafu au waliohai wasiokuwako mbele yako ambao hawawezi kukuokoa. Kitendo hichi ni shirki. Kwa sababu hili linafanywa tu na mtu anayeamini ya kwamba watu hawa wana uendeshaji wa kisiri juu ya ulimwengu na kwa ajili hiyo anakuwa amewapa sehemu katika uola wa Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Ni nani anayemuitika aliyedhikika anapomwomba, akamuondoshea dhiki na akakufanyeni makhalifa ardhini? Je, yuko mungu mwengine pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka.” (an-Naml 27 : 62)

3- Kuwaomba uokozi waliohai, wajuzi na wana uwezo juu ya kukusaidia. Kitendo hichi kinafaa kama jinsi inavyojuzu kuwaomba msaada. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ

”Akamsaidia yule ambaye ni katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake. Muusa akampiga ngumi akamuua papohapo.” (al-Qaswasw 28 : 15)

4- Ni kumuomba uokozi kiumbe aliehai asiyekuwa na uwezo wa kuokoa pasi na kuamini ya kwamba ana uwezo wa kisiri. Kwa mfano mtu yuko katika hali ya kuzama na akamuomba uokozi mtu ambaye amepooza. Hili ni upuuzi, bali ni kumchezea shere yule mpoozaji, jambo ambalo linapaswa kukatazwa. Sababu nyingine ni kwamba yule mzamaji huenda akamghuri mtu mwingine aliyeko pale  ya kwamba mpoozaji huyu ana nguvu za kisiri anazotumia kuoa katika hali ya majanga.

[1]  Muslim (1763) na at-Tirmidhiy (3276).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 27/05/2020