42. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika, na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖفَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa kama tandiko na mbingu kuwa kama paa na akateremsha kutoka mbinguni maji akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki kwenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika, na hali ya kuwa nyinyi mnajua.” (al-Baqarah 02:22)

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Washirika ni shirki ambayo imejificha zaidi kuliko mdudu mchungu apitae juu ya jiwe jeusi katika usiku wenye giza. Nako ni kusema: “Naapa kwa jina la Allaah na kwa uhai wako fulani na uhai wangu”, “Lau ama si kijibwa hiki mwizi angelituingilia”, “Lau kama si bata ya nyumbani wezi wangelituingilia” na mtu kumwambia mwenzake: “Akitaka Allaah na wewe” na mtu kusema pia: “Lau kama si Allaah na fulani”. Usimchanganye Allaah na mwingine yeyote. Yote haya ni kumshirikisha Allaah.

Ameipokea Ibn Abiy Haaatim.

3- ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah amekufuru au ameshirikisha.”[1]

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha na al-Haakim pia ameisahihisha.

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuapa kwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kusema uongo inapendeza zaidi kwangu kuliko kuapa kwa asiyekuwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kusema ukweli.”

5- Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msisemi “Akitaka Allaah na fulani”. Lakini semeni: “Akitaka Allaah kisha akataka fulani”.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

6- Imekuja kutoka kwa Ibraahiym an-Nakha-iy ya kwamba alikuwa akichukia mtu kusema: “Najilinda kwa Allaah na kwako”, lakini alikuwa anajuzisha kusema: “Najilinda kwa Allaah kisha kwako”. Pia akijuzisha mtu kusema: “Lau kama si kwa ajili ya Allaah kisha fulani” na wala usisemi: “Lau kama si kwa ajili ya Allaah na fulani”.

MAELEZO

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖفَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa kama tandiko na mbingu kuwa kama paa na akateremsha kutoka mbinguni maji akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki kwenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika, na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Katika mlango huu mtunzi wa kitabu anachotaka ni kuwatahadharisha watu kumfanyia Allaah washirika. Washirika ni wingi wa mshirika na walinganizi. Allaah amewaita waungu kama makaburi, miti na sayari kuwa ni “washirika” kwa sababu watu wanawaabudu pamoja na Allaah. Kama mtu anakiomba kitu, anakiomba uokozi, anakiomba mambo mengine na anaamini kuwa kinanufaisha na kudhuru kinaitwa “mshirika”. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“… na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Bi maana na nyinyi mnatambua kuwa Yeye ndiye Muumbaji, Mruzukaji na Mungu wa haki (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema wakati alipokuwa akiwasema vibaya baadhi ya watu:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ

“Miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah kuwa ni mungu mshirika ambapo wanawapenda kama mapenzi wanavyompenda Allaah… “ (al-Baqarah 02:165)

Lengo kwa haya ni kuwaita watu kumtakasia ´ibaadah Allaah (Ta´ala) pekee. Yeye ndiye awe Mungu wa haki wa kuabudiwa pekee. Amesema (Ta´ala):

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Mungu wenu ni Mungu mmoja pekee; hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.” (al-Baqarah 02:163)

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.” (al-Mu´minuun 23:117)

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Washirika ni shirki ambayo imejificha zaidi kuliko mdudu mchungu apitae juu ya jiwe jeusi katika usiku wenye giza. Nako ni kusema: “Naapa kwa jina la Allaah na kwa uhai wako fulani na uhai wangu”, “Lau ama si kijibwa hiki mwizi angelituingilia”, “Lau kama si bata ya nyumbani wezi wangelituingilia” na mtu kumwambia mwenzake: “Akitaka Allaah na wewe” na mtu kusema pia: “Lau kama si Allaah na fulani”. Usimchanganye Allaah na mwingine yeyote. Yote haya ni kumshirikisha Allaah.

Ameipokea Ibn Abiy Haaatim.

Ibn ´Abbaas ameyafasiri yote hayo kuwa ni shirki. Anamaanisha kuwa ni shirki ndogo iliyofichikana. Kwa sababu shirki ndogo ndani yake kunaingia kufanya washirika. Lakini baya na khatari zaidi ni kuyaomba masanamu na mawe. Hii ni shirki kubwa. Mtu anatakiwa kutia akilini kwamba shirki iliyofichikana (yaani shirki ndogo) inapelekea katika shirki kubwa. Kwa ajili hiyo ndio maana akazindua juu ya hilo ili watu waweze kujitenga mbali na yote mawili. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoambiwa “Akitaka Allaah na wewe” akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, umenifanya kuwa mshirika wa Allaah? Sema: “Akitaka Allaah pekee.”[3]

Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaonelea kusema “Akitaka Allaah na wewe” ni katika kumfanyia Allaah washirika. Kwa ajili hiyo ndio maana inatakiwa kwa mtu kujiepusha na mambo kama hayo na misemo kama hiyo, kwa sababu “wa” inafahamisha ushirikiano na usawazishaji. Kadhalika inahusiana na msemo “Lau kama si bata au mbwa nyumbani basi watu wa nyumbani wasingeliwatambua wageni”. Ni kosa. Badala yake unatakiwa kusema “Lau kama si Allaah kisha bata”. Allaah ndiye Mwenye kusababisha sababu. Mtu hatakiwi kutegemea sababu; anatakiwa amtegemee Allaah pekee. Kwa ajili hiyo zile sababu hazitakiwi kutajwa peke yake au kuambatanishwa pamoja na “na”, isipokuwa ziambatanishwe na “kisha/halafu”. Mfano wa usemi mwingine ni “Lau kama si mtu yule basi alikuwa azame.” Ni kosa. Bali inatakiwa kusemwa “Lau kama si Allaah kisha fulani basi angelizama”.

 3- ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah amekufuru au ameshirikisha.”[4]

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha na al-Haakim pia ameisahihisha.

Ukweli wa mambo ni kwamba Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ndiye kasimulia haya. Mashaka katika Hadiyth inawezekana yanatokamana na Ibn ´Umar au mpokezi mwingine. Lakini maana yake ni moja. Kuapa kwa jina la mwingine asiyekuwa Allaah ni kumuadhimisha na kuona kuwa mtu/kitu hicho ni chenye kustahiki kiapo hicho. Kwa ajili hiyo inatakiwa kuapa kwa jina la Allaah pekee kwa sababu Yeye ndiye Mwenye kujua siri na mambo yaliyofichikana.

Hapo kabla waarabu walikuwa wakiapa kwa baba zao na kwa watu wakuu. Ni jambo lililokuwa linafaa mwanzoni mwa Uislamu. Kisha baadaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalikataza na kulitahadharisha. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiape kwa baba zenu, mama zenu wala washirika.”[5]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutaka kuapa basi aape kwa Allaah au anyamaze.”[6]

Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa ´Umar kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutaka kuapa basi aape kwa Allaah au anyamaze. Mwenye kuapa kwa kitu kingine badala ya Allaah ameshirikisha.”

Haya ni matamshi ya ´Umar kama tulivosema.

Kitendo hichi ni shirki ndogo. Kuna uwezekano vilevile ikawa ni shirki kubwa ikiwa yule muapaji anaonelea kuwa mtu huyo anayemuapia ana hadhi, anaendesha ulimwengu au anastahiki kuabudiwa badala ya Allaah. Vinginevyo ni shirki ndogo. Kwa ajili hiyo imepokelewa kwamba Salaf walikuwa wakiapa kwa baba zao mwanzoni mwa Uislamu. Lakini kwa ajili ya kukamilisha Tawhiyd, kumuadhimisha Allaah na kufunga njia zote zinazopelekea katika shirki wakayakataza hayo.

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuapa kwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kusema uongo inapendeza zaidi kwangu kuliko kuapa kwa asiyekuwa Allaah hali ya kuwa ni mwenye kusema ukweli.”

Kwa sababu kuapa kwa asiyekuwa Allaah ni shirki na kuapa kwa kuapa kwa Allaah kwa kusema uongo ni dhambi. Shirki ni jambo la khatari kuliko dhambi. Sampuli ya shirki ni khatari kuliko sampuli ya maasi. Pamoja na hivyo uongo pia ni haramu.

5- Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msisemi “Akitaka Allaah na fulani”. Lakini semeni: “Akitaka Allaah kisha akataka fulani”.”[7]

Ameipokea Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Kwa sababu “na” inafahamisha ushirika na usawazishaji. Kwa ajili hiyo haijuzu kusema hivo. Hata hivyo inafaa kusema “kisha/halafu” kwa sababu inaonyesha tofauti. Hata hivyo bora zaidi ni kusema “Lau kama si Allaah pekee.”

6- Imekuja kutoka kwa Ibraahiym an-Nakha-iy ya kwamba alikuwa akichukia mtu kusema: “Najilinda kwa Allaah na kwako”, lakini alikuwa anajuzisha kusema: “Najilinda kwa Allaah kisha kwako”. Pia akijuzisha mtu kusema: “Lau kama si kwa ajili ya Allaah kisha fulani” na wala usisemi: “Lau kama si kwa ajili ya Allaah na fulani”.

Haijuzu kusema “Najilida kwa fulani na fulani” au “Najilinda kwa Allaah na fulani na fulani”. Badala yake sema “Najilinda kwa Allaah”. Huu ndio ukamilifu wa Tawhiyd. Ni wajibu kwa muislamu kutilia bidii juu ya ukamilifu wa Tawhiyd na imani na kujiepusha na aina zote za shirki. Ni wajibu vilevile kujiepusha na sampuli zote za maasi kwa sababu ni mambo yanaipunguza Tawhiyd, imani na yakini.

Faida:

Hadiyth inayosema “Naapa kwa baba yangu atafaulu”[8] ni jambo lilitokea mwanzoni mwa Uislamu na kabla ya kukatazwa kusema hivo.

Haijuzu kusema “Lau kama si Allaah kisha Mtume wake basi tusingeongoka.”

Hadiyth inayosema “Hamwogopi isipokuwa Allaah na mbwa mwitu”[9] ni jambo haliingii katika maudhui haya. Inajuzu.

Haijuzu kusema “Nakuuliza kwa dhimma yako” au “Nakuuliza kwa amana” ikiwa mtu amekusudia kuapa kwa vitu hivyo. Vinginevyo inajuzu.

Inajuzu kusema “Naomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na wewe”. Pindi mwanamke alipomwambia hivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia mwanamke yule:

“Umeomba ulinzi kwa aliye Mtukufu.”[10]

Baada ya hapo akamwacha.

Mtu akitendewa wema na mwengine na akamwambia kwamba yeye ni mwokozi mkubwa, yote haya yanategemea nia. Bora ni kusema “Lau kama isingelikuwa Allaah kisha wewe”. Kusema “Wewe ni mwokozi mkubwa” ni jambo linaweza kuleta mashaka.

[1] Abu Daawuud (3251), at-Tirmidhiy (1535) na Ahmad (6072). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2561).

[2] Abu Daawuud (4980), Ahmad (23313) na Ibn Abiy Shaybah (2669). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (137).

[3] Ahmad (1839), al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (783) na at-Twabaraaniy (13005). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (139).

[4] Abu Daawuud (3251), at-Tirmidhiy (1535) na Ahmad (6072). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2561).

[5] Abû Daawuud (3248) na an-Nasaa’iy (3769). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (7249).

[6] al-Bukhaariy (2679) na Muslim (1646).

[7] Abu Daawuud (4980), Ahmad (23313) na Ibn Abiy Shaybah (2669). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (137).

[8] Muslim (11).

[9] al-Bukhaariy (3852).

[10] al-Bukhaariy (5254).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 132-135
  • Imechapishwa: 01/11/2018