41. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) “Wanazielewa vyema neema za Allaah, kisha wanazikanusha – na wengi wao ni makafiri”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يَعْرِفُونَ نِعْمَتَ اللّهِ ثُمَّ يُنكِرُونَهَا وَأَكْثَرُهُمُ الْكَافِرُونَ

”Wanazielewa vyema neema za Allaah, kisha wanazikanusha – na wengi wao ni makafiri.” (an-Nahl 16:83)

2- Mujaahid amesema kuhusu maana yake:

“Ni mtu kusema: “Hii ni mali yangu. Nimeirithi kutoka kwa mababu zangu.”

3- ´Awn bin ´Abdillaah amesema:

Wanasema:  “Lau  kama si fulani nisingelikuwa hivi na hivi.”

4- Ibn Qutaybah amesema:

“Wanasema: “Haya ni kutokana na uombezi wa waungu wetu.”

5- Abul-´Abbaas amesema baada ya Hadiyth ya Zayd bin al-Haarith:

“Katika asubuhi hii kuna baadhi ya waja Wangu wamepambaukia wakiwa ni wenye kuniamini na wengine wamekufuru. Ama yule aliyesema kwamba: “Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah”, basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari. Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”

“Haya yamekuja sehemu nyingi katika Qur-aan na Sunnah; Allaah (Subhaanah) anawasema vibaya wale ambao wanazinasibisha neema Zake kwa asiyekuwa Yeye na wanamshirikisha.”

6- Baadhi ya Salaf wamesema:

“Aayah inawazungumzia wale wenye kusema: “Upepo ulikuwa mzuri na baharia huyu alikuwa hodari” na mfano wa maneno kama hayo ambayo hupitika katika ndimi za watu wengi.”

MAELEZO

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

يَعْرِفُونَ نِعْمَتَ اللّهِ ثُمَّ يُنكِرُونَهَا وَأَكْثَرُهُمُ الْكَافِرُونَ

”Wanazielewa vyema neema za Allaah, kisha wanazikanusha – na wengi wao ni makafiri.”

Mwandishi amechokusudia ni watu wazitambue neema za Allaah (Subhaanah) na wamshukuru Yeye kwa ajili yazo kwa sababu watu wengi wanaghafilika juu ya hilo. Wanastareheka na neema za Allaah lakini pamoja na hivyo hawamshukuru. Bali wanazinasibisha neema hizo kwa sababu yazo na kwa nguvu zao wenyewe na matendo yao na wakati huohuo wanaghafilika Naye ambaye kihakika ndiye kawatunukia neema hizi. Lau Allaah angelitaka basi angelitokomeza sababu na nguvu ya neema hizo. Allaah ndiye ambaye kamtunukia mtu huyo usikizi, uoni, akili, werevu na mengineyo. Hii ni moja katika tabia za makafiri ambao husema kuwa wamepata mali kwa sababu ya mirathi na mengineyo. Allaah (Ta´ala) amesema:

 ثُمَّ يُنكِرُونَهَا

“… kisha wanazikanusha… “

Wanastareheka nazo na wanazitambua vyema, halafu pamoja na yote haya wanazinasibisha kwa waungu na masanamu yao. Hawataki kuzikiri.

 2- Mujaahid amesema kuhusu maana yake:

“Ni mtu kusema: “Hii ni mali yangu. Nimeirithi kutoka kwa mababu zangu.”

Anasema hivo kwa kujisifu na kujiona juu ya jambo hili pasi na kuzikiri neema za Allaah na anaghafilika na hilo. Hasemi hivo kwa njia ya kuelezea, bali anasema hivo kwa kughafilika na kusahau kwamba ni Allaah kweli ndiye kamtunukia neema hiyo. Hata hivyo ni jambo linalofaa mtu akaelezea sababu ya neema fulani.

3- ´Awn bin ´Abdillaah amesema:

Wanasema:  “Lau  kama si fulani nisingelikuwa hivi na hivi.”

Hili pia ni kosa. Mtu anatakiwa kusema:

“Lau kama si Allaah kisha hivi na hivi… “

Neema inatakiwa kunasibishwa kwa Alallah. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye mwenye kutoa na kutunuku.

4- Ibn Qutaybah amesema:

“Wanasema: “Haya ni kutokana na uombezi wa waungu wetu.”

Haya ni maneno ya makafiri. Ni wajibu kwa muislamu kujitofautisha nao na kuzinasibiha neema kwa Allaah. Allaah ndiye Mwenye kusababisha sababu. Kwa ajili hiyo ni wajibu kwa muislamu kumshukuru Allaah na kuyatendea kazi maamrisho Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ۖ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ

“Neema yoyote mliyo nayo, basi ni kutoka kwa Allaah. Kisha inapokuguseni dhara Kwake mnamlilia msaada.”[1]

5- Abul-´Abbaas amesema baada ya Hadiyth ya Zayd bin al-Haarith:

“Katika asubuhi hii kuna baadhi ya waja Wangu wamepambaukia wakiwa ni wenye kuniamini na wengine wamekufuru. Ama yule aliyesema kwamba: “Tumenyeshewa mvua kwa fadhila na rehema ya Allaah”, basi huyo ndiye aliyeniamini Mimi na amekufuru sayari. Ama yule aliyesema ya kwamba tumenyeshewa mvua kutokana na sayari fulani na fulani, basi huyo amenikufuru Mimi na ameamini sayari.”

“Haya yamekuja sehemu nyingi katika Qur-aan na Sunnah; Allaah (Subhaanah) anawasema vibaya wale ambao wanazinasibisha neema Zake kwa asiyekuwa Yeye na wanamshirikisha.”

 Wanasema hivo kwa kujisifu na kujitapa mbele za wengine.

6- Baadhi ya Salaf wamesema:

“Aayah inawazungumzia wale wenye kusema: “Upepo ulikuwa mzuri na baharia huyu alikuwa hodari” na mfano wa maneno kama hayo ambayo hupitika katika ndimi za watu wengi.”

Wanasema hivo pindi safina inaporudi salama salimina. Wanamsahau Allaah kwamba ndiye ambaye aliwapa upepo huo na ndiye ambaye kamfunza baharia huyo. Kwa hivo ni wajibu kuzinasibisha neema kwa Allaah (Ta´ala) pamoja na kuzitambua sababu kama vile kusema kwamba Allaah katusahalishia upepo mzuri. Hili linafaa. Hii ni dalili inayoonyesha namna ambavo Salaf walikuwa wakitilia bidii na kupupia juu ya kumshukuru Allaah na kuzitambua neema Zake (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 16:53

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 130-131
  • Imechapishwa: 01/11/2018