42. Kuwazika wafu misikitini ni njia inayopelekea katika shirki

Kwa jina la Allaah. Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na wale watakaoshikana na mwongozo wake.

Amma ba´d:

Nimesoma gazeti la Khartoum lililotolewa tarehe 04/17/1415 H ambapo kumeenezwa ubainifu wa kuzikwa bwana Muhammad al-Hassaan al-Idriys pembezoni na baba yake katika msikiti wao katika mji wa Omdurman…

Wakati Allaah alipowajibisha kuwapa nasaha kwa waislamu na kubainisha kukemea maovu ndipo nikaona nizindue kwamba kuzika msikitini ni jambo lisilojuzu. Bali ni njia inayopelekea katika shirki na ni miongoni mwa matendo ya mayahudi na manaswara ambao wamesimangwa na Allaah juu yake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawalaani. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.” [1]

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jundub bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya kufa kwake kwa siku tano akisema:

“Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[2]

Hadiyth zilizopokelewa zikiwa na maana kama hii ni nyingi.

Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu kila mahali – kuanzia serikali na raia – kumcha Allaah, watahadhari na yale Allaah aliyokataza na wawazike wafu wao nje ya misikiti. Hivo ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) wakiwazika wafu wao nje ya misikiti na vivyo hivyo wale waliowafuata kwa wema.

Kuhusu kuwepo kwa kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ndani ya msikiti wake, sio hoja ya kuwazika wafu ndani ya misikiti. Kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizikwa nyumbani kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kisha wakazikwa marafiki zake pamoja naye. Pindi al-Waliyd bin ´Abdil-Malik alipopanua msikiti ndipo akakiingiza chumba ndani yake mwanzoni mwa miaka mia moja ya mwanzo baada ya kuhajiri. Wanazuoni walimkemea. Lakini aliona kuwa jambo hilo halizuii kupanua na kwamba jambo liko wazi na halitatizi.

Kwa ajili hiyo inamdhihirikia kila muislamu ya kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhumaa) hawakuzikwa ndani ya msikiti. Kuingizwa kwao ndani yake kwa sababu ya kupanua sio hoja ya kufaa kuzika misikitini. Kwa sababu hawako msikitini. Wako nyumbani kwake (´alayhis-Swalaatu wa as-Salaam). Aidha kitendo cha al-Waliyd hakisilihi kuwa hoja kwa yeyote katika kufanya hivo. Hoja inakuwa ndani ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) – tunamuomba atujaalie kuwa katika wale wanaowafuata kwa wema.

Kwa ajili ya kutoa nasana na kutaka dhimmah imehaririwa tarehe 14/05/1415 H.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah zake na wale watakaowafata kwa wema.

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[2] Muslim (532).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 135-137
  • Imechapishwa: 21/07/2022