41. Kusmwalia maiti wakati mtu ameenda kumtembelea

Swali: Je, inafaa kuswalia kaburi la baba yangu swalah ya jeneza wakati ninapomtembelea kwa ajili ya kumwombea rehema? Je, maiti akirithisha msahafu anapata thawabu wakati watoto wake unapousoma?

Jibu: Ikiwa umemswalia baba yako pamoja na wengine basi hakuna haja ya kurudia kuswali mara nyingine. Bali utamtembelea na kumwombea du´aa peke yake. Utaenda makaburi, utawatolea salamu waliyomo makaburini, utawaombea du´aa na kumwombea du´aa baba yako. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwafunza Maswahabah zake pindi wanapoyatembelea makaburi basi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya. Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[2]

Hii ndio Sunnah.

Utawatolea salamu watu wa makaburi na baba yako na utamuombea msamaha na rehema. Hapana haja ya kuswali. Hapa ni pale ambapo utakuwa umemswalia hapo kabla. Lakini ikiwa hukumswalia pamoja na watu wengine basi utaenda makaburini na utamswalia katika kipindi kisichozidi mwezi ikiwa ameshapitisha muda usiyozidi mwezi. Lakini ikiwa muda umesharefuka basi hakuna swalah kwa mujibu wa maoni ya kikosi cha wanazuoni. Katika hali hiyo itatosha kumwombea du´aa baba yako, msamaha, kumtakia rehema na kumtolea swadaqah ya pesa. Yote haya yanamnufaisha baba yako na wengineo.

Kuhusu msahafu ikiwa maiti nyuma yake Waqf wa msahafu basi utamfaa ujira wake. Ni kama ambavo ataacha Waqf wa elimu yenye manufaa; elimu ya Shari´ah au elimu iliyoruhusiwa ambayo watu wananufaika nayo. Basi katika hali hiyo atapewa ujira kwa mambo hayo. Kwa sababu ni kusaidiana katika kheri. Ni kama ambavo ataacha Waqf wa ardhi, nyumba au dukani ambapo anatoa swadaqah chumo lake kuwapa masikini au akajitolea msikiti. Yote haya analipwa ujira kwayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[3]

Swadaqah yenye kuendelea inamfaa maiti akiwa muislamu. Aidha inamfaa du´aa ya watoto wake na du´aa za wengine. Vilevile inamfaa Waqf anayoacha baada yake katika njia ya kheri katika nyumba, ardhi, dukani, mitende na mfano wa mambo hayo. Ananufaika kwa Waqf huu mdua wa kuwa watu wananufaika nayo; wanakula matunda yake na kunufaika na matunda yake au matunda yake yakatumiwa katika misikiti ya waislamu kwa ajili ya kutengeneza au kuimarisha samani zake.

[1] Muslim (976).

[2] Muslim (974).

[3] Muslim (1631).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 133-135
  • Imechapishwa: 21/07/2022