42. Hakuna yeyote atakayeingia Peponi kutokana na matendo yake

Wanaitakidi na kushuhudia ya kwamba hakuna yeyote ambaye inamthubutukia kuingia Peponi, ingawa matendo yake yatakuwa mazuri, akafanya ´ibaadah kwa kumtakasia nia Allaah hali ya juu na utiifu wake ukawa msafi zaidi na njia yake ikapendeza zaidi, isipokuwa ikiwa Allaah atamtunuku, ambapo itamthubutukia kwa fadhilah na neema Zake. Kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) ndiye ambaye amemuwepesishia kufanya hayo matendo mema. Allaah asingemuwepesishia, basi yasingelimkuwia wepesi. Asingemwongoza, basi asingeongoka. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَىٰ مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُزَكِّي مَن يَشَاءُ

”Na lau si fadhilah za Allaah juu yenu na rehema Zake, basi asingelitakasika kati yenu hata mmoja abadani, lakini Allaah anamtakasa amtakaye.”[1]

Ameeleza kuwa wakazi wa Peponi watasema:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَـٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ

”Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye ametuongoza kwa haya, na tusingelikuwa wenye kuongoka kama si Allaah kutuongoza.”[2]

Zipo Aayah zingine nyingi mfano wake.

[1] 24:21

[2] 7:43

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 294-295
  • Imechapishwa: 25/12/2023