Ukishajua hilo, na ukajua ya kwamba ni lazima wawepo maadui ambao wamekaa katika njia ya Allaah, ni watu wenye ufaswaha, elimu na hoja, basi lililo la wajibu kwako ni kujifunza kutoka katika dini ya Allaah kile ambacho itakuwa ni silaha yako ili kuweza kupambana na mashaytwaan hawa ambao kasema kiongozi wao kumwambia Mola Wako (´Azza wa Jall):

لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“Nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka, kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao; na wala Hutopata wengi wao wenye kushukuru.” (al-A´raaf 07 : 16-17)

MAELEZO

Wanaonelea kuwa hoja za Qur-aan na Sunnah ni za kutia dhana. Kwa mujibu wao hazifidishi yakini. Huu ni katika utimilifu wa mtihani na kutaka kuwapaka watu mchanga wa machoni. Kwa kuwa hali halisi ya kweli ni kinyume chake. Nao ni kwamba dalili za Qur-aan zinafidisha yakini. Upande mwingine dalili za mantiki na mijadala zinafidisha kuchanganyikiwa. Hayo yamethibitishwa na wale wakuu wao wakati wa kukata roho na wengine wametubia na kujirudi kutokamana na elimu ya falsafa.

Haikustahikii wewe kukabiliana na watu hawa endapo watakuwa na ufaswaha, hoja na vitabu ilihali huna silaha. Itakuwajibikia kujifunza kutoka katika Qur-aan na Sunnah yale yatayokuwezesha kuzibatilisha hoja za watu hawa ambao Ibliys, kiongozi wao, alimwambia Mola Wako (´Azza wa Jall):

لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ

“Nitawakalia… “

bi maana wanaadamu.

صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ

“… njia Yako iliyonyooka.”

bi maana njia yenye kufikisha Kwako.

ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“… kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao; na wala Hutopata wengi wao wenye kushukuru.” (07:16-17)

Khabithi huyu ameahidi kuwa atajaribu kumpoteza mwanaadamu. Hiyo vilevile ndio kazi inayofanywa na wafuasi wake katika mashaytwaan wa kibinaadamu miongoni mwa wale wenye vitabu vya upotevu na fikira zilizopinda ambapo wanasimama kidete kufanya kazi ya Ibliys katika kuwapotaza watu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 58
  • Imechapishwa: 06/12/2016