41. Dalili kwamba Tawhiyd ndio kubwa aliloamrisha Allaah na shirki ndio kubwa alilokataza

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”[1]

MAELEZO

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”

Tumesema kuwa dalili juu ya kwamba kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd ni maneno Yake (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”

Kisha akataja haki zilizobaki. Kitendo cha Yeye kuanza kutaja Tawhiyd na kukataza shirki ni dalili inayoonyesha kuwa Tawhiyd ndio kubwa aliloamrisha Allaah. Amesema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ

“Mwabuduni Allaah… “

akayafuatiza kwa maneno Yake:

وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“… na wala msimshirikishe na chochote.”

Haya ni makatazo. Akaanza kwa kuamrisha Tawhiyd na kukataza shirki. Kwa hiyo ikajulisha kuwa kubwa aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd na kubwa alilokataza ni shirki. Kwa sababu Allaah ameanza kwa hayo. Haanzi (Subhaanah) isipokuwa kwa kilicho muhimu zaidi kisha yanayofuatia baada ya hapo. Hii ndio namna Aayah ilivyofahamisha.

[1] 04:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 14/12/2020