Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa sifa za Allaah (Ta´ala) ni kuwa anazungumza kwa maneno ya milele na anamsikilizisha yule amtakaye katika viumbe Wake. Muusa (´alayhis-Salaam) aliyasikia kutoka Kwake pasi na mkati kati. Vilevile Jibiriy (´alayhis-Salaam) aliyasikia na vivyo hivyo Malaika wengine aliyowaidhinisha na Mitume Yake. Hakika Yeye (Subhaanah) atawazungumzisha waumini Aakhirah na [wao waumini] watazungumza Naye. Atawapa idhini wamtembelee. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا

”Na bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno kihakika.”[1]

يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي

”Ee Muusa! Hakika Mimi nimekuteua juu ya watu kwa Ujumbe na maneno Yangu.”[2]

مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ

”Miongoni mwao [Mitume kuna] ambaye Allaah alimzungumzisha.”[3]

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ

”Na wala haikuwa kwa mtu yeyote yule kwamba Allaah amsemeze isipokuwa kwa njia ya Wahy au nyuma ya pazia.”[4]

فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ إِنِّي أَنَا رَبُّكَ

“Basi alipoufikia aliitwa: “Ee Muusa! Hakika Mimi ni Mola Wako.”[5]

إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي

”Hakika mimi ni Allaah, hakuna mungu wa haki isipokuwa Yeye, basi niabudu.”[6]

Haijuzu kwa mwengine yeyote kusema haya isipokuwa Allaah Pekee. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Allaah anapotamka kwa Wahy, sauti Yake wanaisikia walioko mbinguni.”[7] Hilo limepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

´Abdullaah bin Unays amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Allaah atawafufua viumbe siku ya Qiyaamah wakiwa uchi, peku, hawakutahiriwa na bila ya kitu na atawanadi kwa sauti watayomsikia walio mbali kama wanavyomsikia walio karibu: “Mimi ndiye mfalme! Mimi ndiye Mwenye kuhukumu!””[8] Imepokelewa na maimamu na al-Bukhaariy ameitumia kama hoja[9].

Katika baadhi ya Aathaar imepokelewa ya kwamba Muusa (´alayhis-Salaam) usiku mmoja aliona moto ambapo akaingiwa na khofu. Hivyo Mola Wake akamwita: “Ee Muusa!” Akaitika kwa haraka na kwa adabu: “Nakuitikia. Nakuitikia. Naisikia sauti Yako lakini sioni ulipo. Uko wapi?” Akasema: “Mimi niko juu yako, mbele yako, kuliani mwako na kushotoni mwako.” Hivyo Muusa akajua kuwa sifa hizi hazimstahikii yeyote isipokuwa Allaah (Ta´ala). Akasema: “Ni Wewe ndiye Mola Wangu. Hivi kweli nasikia maneno Yako Wewe au ni maneno ya Mtume Wako?” Akasema: “Hapana, ni maneno Yangu ee Muusa.”[10]

MAELEZO

15 – Maneno. Maneno ni miongoni mwa sifa za Allaah zilizothibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا

”Na bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno kihakika.”

مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ

”Miongoni mwao [Mitume kuna] ambaye Allaah alimzungumzisha.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapotaka kufunua amri ya jambo fulani, basi huzungumza kwa Wahy.”

 Ameipokea Ibn Khuzaymah, Ibn Jariyr na Ibn Abiy Haatim.

Salaf wameafikiana juu ya kumthibitishia maneno Allaah. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo pasi na kupotosha, kukanusha, kuufanyia namna wala kuupigia mfano. Ni maneno ya ukweli yanayolingana na Allaah na yaliyofungamana na matakwa Yake kwa herufi na sauti inayosikiwa.

Dalili ya kuwa maneno ya Allaah yanatokana na matakwa Yake ni maneno Yake (Ta´ala):

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ

“Na alipokuja Muusa katika miadi Yetu na Mola wake akamsemesha.”[11]

Kuzungumzishwa kumepatikana baada ya kuja kwa Muusa. Hiyo inafahamisha kwamba imefungamana na matakwa Yake (Ta´ala).

[1] 04:164

[2] 07:144

[3] 02:253

[4] 42:51

[5] 20:11- 12

[6] 20:14

[7] Abu Daawuud (4738), Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (95-96), al-Aajurriy katika “ash-Shariy´ah” (294) na wengineo.

[8] Imaam al-Albaaniy amesema katika ”Takhriyj-us-Sunnah”: ”Hadiyth Swahiyh.”

[9] Tazama kitabu ”Adab-ul-Mufrad (970), Khalq Afa´aal-il- ´Ibaad (89) na at-Taariykh al-Kabiyr (7/169) vya al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah). Imekuja pia kwa Ahmad (3/490), al-Haakiym (2/437- 438), al-Bayhaqiy katika “Kitaab-ul-Asmaa´ was-Swifaat” (131) na wengineo.

[10] as-Suyuutwiy katika ”ad-Durr al-Manthuur” (4/290-292), Ibn-ul-Mundhir, Ibn Abiy Haatim na imenasibishwa pia kwa Ahmad “az-Zuhd”.

[11] 07:143

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 69-72
  • Imechapishwa: 26/10/2022