Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Siynaan aliyesema:

“Baada ya kumzika mvulana wangu nikasimama pembezoni mwa kaburi, Abu Twalhah akanishika mkono na kunambia: “Nisikupe bishara njema?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “adh-Dhwahhaak bin ´Abdir-Rahmaan amenieleza kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) husema: “Ee Malaika wa mauti! Umemchukua mtoto wa mja wangu? Umechukua kipumbazo cha macho yake na matunda ya moyo wake?” Ndipo atajibu: “Ndio.” Allaah aseme: “Alisema nini?” Ajibu: “Amekushukuru na kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” Ndipo Allaah aseme: “Mjengee mja Wangu nyumba Peponi na ipeni jina “Nyumba ya shukurani”.”

Hivyo ndivyo alivyopokea at-Tirmidhiy pia na kusema kuwa ni nzuri na geni. Ibn Hibbaan na Ibn ´Asaakir wameipokea kwa matamshi:

“Pindi mtoto wa mja anapofariki Allaah (´Azza wa Jall) huwauliza Malaika Wake: “Mmemchukua mtoto wa mja wangu?” Waseme: “Ndio.” Allaah aseme: “Alisema nini?” Wajibu: “Amekushukuru na kusema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” Ndipo Allaah aseme: “Mjengee mja Wangu nyumba Peponi na ipeni jina “Nyumba ya shukurani”.”

Ahmad amepokea kupitia kwa Mu´aawiyah bin Qurrah aliyesimulia kutoka kwa baba yake ya kwamba kuna mtu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtoto wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Unampenda?” Akajibu: “Ee Mtume wa Allaah! Allaah akupende kama jinsi ninavyompenda.” Ghafla Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa hamuoni yule mtu. Akasema: “Vipi kuhusu mtoto wa fulani?” Wakamwambia: “Amefariki, ee Mtume wa Allaah!” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia baba yake: “Hupendi kuingia moja katika milango ya Peponi na kukuta kuwa anakusubiri?” Mtu mmoja akasema: “Yanamuhusu yeye mwenyewe, ee Mtume wa Allaah, au na sisi pia?” Akajibu: “Yanawahusu nyinyi nyote.” an-Nasaa’iy (1870). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim, adh-Dhahabiy na al-Albaaniy katika ”Ahkaam-ul-Janaa-iz”, uk. 162.

al-Bayhaqiy amepokea kupitia njia nyingine ya kwamba kuna mtu kutoka katika Answaar alisimama na kusema:

“Ee Nabii wa Allaah! Haya yanamuhusu yeye mwenyewe au waislamu wote anayefiwa na mtoto wake?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Yanahusu waislamu wote anayefiwa na mtoto.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 14/10/2016