39. Watu wa Muusa walivyotaka kutumbukia katika shirki

na khaswa Allaah akikuongoza kwa yale Aliyoelezea kuhusu watu wa Muusa – pamoja na wema wao na elimu yao – walipomuendea na kumwambia:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana mungu!” (al-A´raaf 07: 138)

hapo ndipo khofu na bidii yako itaongezeka kwa yale yatakayokuokoa kutokana na haya na mfano wake.

MAELEZO

Watu wa Muusa ni Banuu Israaiyl waliomuamini Muusa na wakatoka pamoja naye pindi Allaah alipomuamrisha awatoe kwa ajili ya kumkimbia Fir´awn. Jambo lili liliwafichika pamoja na kuwa kati yao walikuwepo wasomi, wema na wachaji. Wakatoka pamoja na Muusa kwa kumkata Fir´awn na watu wake. Walipofika kwa watu waliokuwa wakikaa kwa muda mrefu kwenye masanamu yao ndipo wakataka kuwafuata kichwa mchunga na wakamuomba Muusa kwa kusema:

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

”Tufanyie nasi mungu kama walivokuwa hawa wana mungu!” (07:138)

Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawakemea kwa maneno haya na akawajuza kuwa kitendo cha watu hawa ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Tazama namna ambavyo jambo hili lilifichikana kwao. Haya yanathibitisha ukhatari wa kuwa na ujinga juu ya Tawhiyd na kutotambua uhakika wa shirki. Hayo ni miongoni mwa sababu zinazompelekea mtu kutamka neno linalopelekea katika kufuru na kutoka katika Uislamu pasi na yeye kujua. Hakuna kitachokuokoa kutokamana na haya na mfano wake isipokuwa elimu yenye manufaa ambayo itakujulisha Tawhiyd kutokamana na shirki na kukuhadharisha na maneno au matendo yanayoweza kukutumbukiza katika shirki pasi na wewe kujua. Haya yanathibitisha ubatilifu wa wale wenye kusema kuwa mtu mwenye kusema neno la kufuru au kitendo cha kufuru hawezi kukufuru mpaka aamini yale ima aliyoyasema au kuyatenda moyoni mwake. Vilevile yanabatilisha maneno ya wale wenye kusema kuwa mjinga anapewa udhuru kwa njia isiyofungamana hata kama atakuwa na uwezo wa kuuliza na kujifunza. Haya ni maneno ya baadhi ya wale wenye kujinasibisha na elimu na Hadiyth hii leo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqarunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 55
  • Imechapishwa: 01/12/2016