Swali 39: Tunatumai utuwekee wazi namna ya kuswalia jeneza kama ilivyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kwani watu wengi hawajui[1].

Jibu: Sifa ya kuswalia jeneza ni jambo amelibainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Mosi anatakiwa kusema “Allaahu Akbar”, aombe kinge dhidi ya shaytwaan aliyefukuzwa mbali, aseme “Bismillaahi ar-Rahmaan ar-Rahiym”, asome al-Faatihah na Suurah nyingine fupi au baadhi ya Aayah, kisha aseme “Allaahu Akbar” na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama anavomswalia mwishoni mwa swalah, kisha aseme “Allaahu Akbar” mara ya tatu na amwombee du´aa maiti. Du´aa bora ni yeye aseme:

اللهم اغفر لحينا وميتنا، وشاهدنا وغائبنا، وصغيرنا وكبيرنا، وذكرنا وأنثانا، اللهم من أحييته منا فأحيه على الاسلام، ومن توفيته منا فتوفه على الايمان، اللهم لا تحرمنا أجره، ولا تضلنا بعده اللهم اغفر له وارحمه، وعافه واعف عنه، وأكرم نزله، ووسع مدخله واغسله بالماء والثلج والبرد، ونقه من الخطايا كما ينقى الثوب الأبيض من الدنس اللهم أبدله دارا خيرا من داره وأهلا خيرا من أهله، اللهم أدخله الجنة وأعذه من عذاب القبر ومن عذاب النار، وافسح له في قبره ونور له فيه، اللهم لا تحرمنا أجره ولا تضلنا بعده

“Ee Allaah! Msamehe aliyehai katika sisi na aliyekufa katika sisi, aliyepo na asiyekuwepo, wadogo wetu na wakubwa wetu, wakiume wetu na wakike wetu.  Ee Allaah! Ambaye utampa uhai katika sisi basi mpe uhai katika Uislamu na utayemfisha katika sisi basi mfishe juu ya imani.  Ee Allaah! Usitunyime ujira Wake na wala usitupoteze baada ya yeye kuondoka. Ee Allaah! Mghufurie na mrehemu, muafu na msamehe na mtukuze kushuka kwake [kaburini] na mpanulie maingilio yake na muoshe na maji na kwa theluji na barafu na mtakase na makosa kama Ulivyoitakasa nguo nyeupe kutokamana na uchafu. Ee Allaah! Mbadilishie nyumba bora kuliko nyumba  yake na jamaa bora kuliko jamaa zake. Ee Allaah! Mwingize Peponi na mlinde kutokamana na adhabu ya kaburi na adhabu ya Moto. Mpanulie kaburi lake na muwekee nuru ndani yake. Ee Allaah! Usitunyime ujira wake na usitupoteze baada yake.”

Yote haya yamehifadhiwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akimwombea du´aa nyengine ni sawa. Mfano anaweza kusema:

اللهم إن كان محسنا فزد في إحسانه وإن كان مسيئا فتجاوز عن سيئاته، اللهم اغفر له وثبته بالقول الثابت

 “Ee Allaah! Akiwa ni mwema basi mzidishie katika mema yake na akiwa ni muovu msamehe makosa yake. Ee Allaah! Mghufurie na mthibitishe kwa kauli thabiti.”

Kisha aseme “Allaahu Akbar” mara ya nne na asimame kidogo, kisha alete Tasliym moja upande wa kuliani mwake hali ya kusema:

السلام عليكم ورحمة الله

“Amani na rehema za Allaah ziwe juu yenu.”

Imesuniwa kwa imamu kusimama usawa na kichwa cha mwanamme na usawa na katikati na mwanamke. Hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa Anas na Samurah bin Jundub (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Kuhusu maneno ya baadhi ya wanazuoni wanaosema kuwa Sunnah ni kusimama usawa na kifua cha mwanamme ni maoni dhaifu. Hayana dalili kutokana na ninavojua. Maiti wakati anaposwaliwa anatakiwa kuelekezwa upande wa Qiblah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Ka´bah:

“Ni Qiblah chenu mliohai na wafu.”[2]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/141-142).

[2] Abu Daawuud (2874).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 20/12/2021