386. Je, inafaa kusema kuwa mtu fulani amerehemewa?

Swali 386: Je, inafaa kusema kuwa mtu fulani amerehemewa (المرحوم فلان)?

Jibu: Ikiwa mtu anasema kuwa maiti amerehemewa, amesamehewa na kadhalika kwa lengo la kuthibitisha, haijuzu. Kwa sababu hajui kama amesamehewa kikweli au hakusamehewa. Haijuzu kwa mtu kusema kwa kukata kwa kitu ambacho hakitambuliki, kwa sababu huko ni kumshuhudia rehema na msamaha pasi na elimu. Kutoa ushahidi pasi na elimu ni jambo la haramu.

Lakini ikiwa anasema hivo kwa njia ya kutarajia kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anamrehemu, hapana vibaya. Hakuna tofauti ya kusema “mrehemewa” (المرحوم) au “Allaah amrehemu” (رحمه الله) kwa sababu maneno yote mawili yanaweza kutumika kwa njia ya kuthibitisha na kuomba du´aa. Kwa hivyo inategemea na nia ya mtamkaji. Wale wanaosema kuwa fulani amerehemwa au amesamehewa hawakusudii kumtolea ushahidi yule maiti kwamba amerehemewa au amesamehewa; wanasema hivo kwa ajili ya kutarajia, dhana njema na du´aa. Kwa hivyo hakuna vibaya kusema hivo.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/451)
  • Imechapishwa: 14/06/2026