38. Ulazima wa mswaliji kusoma al-Faatihah na kuhusu kinyamazo cha imamu baada ya al-Faatihah

Swali 38: Yametofautiana maoni ya wanazuoni kuhusu kisomo cha anayeongozwa na imamu. Ni yepi maoni ya sawa juu ya hilo? Je, analazimika kusoma al-Faatihah? Ni lini ataisoma ikiwa imamu hakufanya kinyamazo kidogo kitachowafanya maamuma kuweza kuisoma? Je, imesuniwa kwa imamu kunyamaza kidogo baada ya kumaliza kusoma al-Faatihah ili kuwawezesha maamuma kusoma al-Faatihah?

Jibu: Maoni ya sawa ni ulazima wa kusoma al-Faatihah kwa mswaliji katika swalah zote za kusoma kimyakimya na swalah za kusoma kwa sauti ya juu. Hilo ni kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hana swalah yule ambaye hakusoma ufunguzi wa Kitabu.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Huenda mnasoma nyuma ya imamu wenu?” Tukajibu: “Ndio.” Akasema: “Msifanye hivo isipokuwa ufunguzi wa Kitabu. Kwani hana swalah yule ambaye hakuisoma.”

Ameipokea Imaam Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

Kilichowekwa katika Shari´ah ni yeye kuisoma wakati imamu anaponyamaza. Imamu asiponyamaza aisome hata kama imamu anasoma kisha akimaliza anyamaze. Hili ni lenye kubaguliwa kutoka katika ueneaji wa dalili zinazofahamisha kuhusu ulazima wa kunyamaza wakati imamu anaposoma. Lakini iwapo imamu atasahau au akaacha kwa ujinga au kwa kuona kuwa sio lazima basi hakuna kitu juu yake na kitamtosha kisomo cha imamu kwa mtazamo wa wanazuoni wengi. Vivyo hivyo pale atakapokuja na kumkuta imamu amerukuu basi atarukuu pamoja naye na kisomo kitadondoka kwake yeye kwa sababu ya kutomuwahi. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti katika Hadiyth ya Abu Bakrah ath-Thaqafiy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ya kwamba alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkuta amerukuu ambapo na yeye akarukuu nje ya safu. Kisha akajiunga ndani ya safu. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotoa salamu akamwambia:

“Allaah akuzidishie pupa na usirudie.”

Hakumwamrisha kulipa Rak´ah nyingine. Hadiyth hii ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

Maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na usirudie.”

ni kuwa usirudie kurukuu nje ya safu. Kwa hayo inapata kujulikana kuwa ambaye ataingia msikitini akamkuta imamu amerukuu basi asirukuu kabla ya safu. Ni lazima kwake kusubiri mpaka atapofika katika safu ijapo itampita Rukuu´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtapoijilia swalah basi tembeeni na lazimianeni na utulivu. Kile mtachowahi kiswalini na kile kitachokupiteni kikamilisheni.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Kuhusu Hadiyth isemayo:

“Ambaye yuko na imamu basi kisomo chake [imamu] ndio kisomo chake [maamuma].”

ni dhaifu. Wanazuoni hawaijengei hoja. Hata kama imesihi basi al-Faatihah ni yenye kubaguliwa kutokana na hayo kwa ajili ya kuoanisha Hadiyth zote.

Kuhusu kinyamazo kidogo baada ya al-Faatihah hakukusihi juu yake chochote kutokana na ninavojua. Lakini jambo ni lenye wasaa – Allaah akitaka. Ambaye atafanya hivo ni sawa na ambaye ataacha kufanya hivo ni sawa. Kwa sababu hakukuthibiti chochote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na ninavojua. Kilichothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni vinyamazo viwili:

1 – Baada ya Takbiyrat-ul-Ihraam ambapo ndani yake inapendeza kusoma du´aa ya kufungulia swalah.

2 – Baada ya kumaliza kusoma kabla ya yeye kwenda katika Rukuu´. Ni kinyamazo kidogo ambacho kinapambanua kati ya kisomo na Takbiyr.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 29/08/2022