Swali 37: Waislamu wengi hii leo wanachukulia wepesi kuswali kwa mkusanyiko mpaka baadhi ya wanafunzi. Wanatoa sababu kuwa baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba sio lazima. Ni ipi hukumu ya swalah ya mkusanyiko? Ni kipi unachowanasihi watu hawa?

Jibu: Kuswali kwa mkusanyiko pamoja na waislamu misikitini ni lazima pasi na shaka yoyote kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni kwa kila mwanamme, muweza na ambaye anasikia adhaana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesikia wito na asiutikie basi hana swalah isipokuwa kutokana na udhuru.”

Ameipokea Ibn Maajah, ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na al-Haakim kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliulizwa: “Ni upi udhuru?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bwana mmoja kipofu alikuja na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimetamani niamrishe kuswaliwe ambapo ikasimamishwa kisha nikamwamrisha mtu awaswalishe watu halafu nikaondoka na kikosi cha wanamme walio na vifurushi vya kuni kuwaendea watu ambao hawashuhudii swalah nikazichoma nyumba zao kwa moto.”

Hadiyth hizi zote na nyinginezo zilizo na maana kama hiyo zinafahamisha ulazima wa wanamme kuswali katika mkusanyiko misikitini na kwamba mwenye kuacha kufanya hivo anastahiki kuadhibiwa vikali. Kama kuswali kwa mkusanyiko misikitini ingelikuwa sio lazima basi mwenye kuiacha asingelistahiki kuadhibiwa.

Isitoshe kuswali kwa mkusanyiko ni miongoni mwa nembo kubwa na zenye kuonekana za Uislamu ikiwa ni pamoja na waislamu kujuana, kupendana na kuondoka kwa vifundo. Jengine ni kwamba kuiacha ni kujifananisha na wanafiki. Kwa hivyo kilicho lazima ni kutahadhari jambo hilo. Tofauti iliopo si yenye kuzingatiwa. Kila maoni yanayoenda kinyume na dalili za ki-Shari´ah ni lazima kuyatupilia mbali na yasizingatiwe. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[1]

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ

”Jambo lolote lile mlilokhitilafiana kwalo, basi hukumu yake ni kwa Allaah. Huyo ndiye Allaah, Mola wangu, Kwake nategemea na Kwake narejea kutubia.”[2]

Katika “Swahiyh” ya Muslim kutoka kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´an) aliyesema:

“Tulikuwa tukijiona hakuna anayeiacha kuswali kwa mkusanyiko isipokuwa ni mnafiki ambaye unatambulika unafiki wake au mgonjwa. Mtu alikuwa akibebwa kati ya watu wawili mpaka anasimamishwa katika safu.”

Hapana shaka kwamba haya yanafahamisha namna ambavo Maswahabah walikuwa wakitilia umuhimu kuswali kwa mkusanyiko msikitini na kupupia kwao kiasi cha kwamba baadhi ya nyakati humleta mtu ambaye ni mgonjwa akabebwa kati ya watu wawili mpaka akasimamishwa kidete katika safu. Hilo ni kutokana na kutilia kwao mkazo kuswali kwa mkusanyiko – Allaah awawie radhi wote.

[1] 04:59

[2] 42:10

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 29/08/2022