38. Radd juu ya wenye kuacha matendo mema kwa hoja ya Qadar

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna yeyote awezaye kuiepuka Qadar iliyopangwa na wala havuki kile alichoandikiwa katika Ubao ulioandikwa.

MAELEZO

Vivyo hivyo Shaykh (Rahimahu Allaah) na Ahl-us-Sunnah wanaamini ya kwamba hakuna mtu awezaye kuepuka mipango na makadiro ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amemkadiria. Hilo ni tofauti na Mu´tazilah wenye kusema kuwa mja anaweza kufanya pasi na Allaah kuwa na matakwa.

Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa Allaah (Subhaanah) anamkadiria mja mitihani na majaribio kwa ajili amlipe thawabu au amuadhibu. Anaweza kumkadiria mja mambo kwa ajili ya kumuadhibu. Mja anafanya sababu na Allaah (Jalla wa ´Alaa) anazipangia sababu hizo natija. Akifanya sababu nzuri basi Allaah anampangia natija nzuri na akifanya sababu za haramu basi Allaah anampangia natija mbaya. Amesema (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa [mali zake] na akamcha Allaah na akasadikisha al-Husnaa, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi.”[1]

Sababu inatokana na mja na natija inatokana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Anawalipa thawabu watenda mema na anawafanyia wepesi na kuwasaidia yale mambo mepesi. Anawaadhibu watenda maasi. Anawaacha na kuwamakinisha juu ya matendo hayo kwa ajili ya kuwaadhibu kwa ajili awachukulie hatua na awaadhibu kwa sababu ya nia zao mbaya na kwa sababu ya mienendo yao:

وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ  فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ

“Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha al-Husnaa, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.”[2]

Mja ndiye mwenye kusababisha na Allaah anamkadiria natija ya matendo yake na nia yake yeye; ima thawabu au adhabu. Kwa ajili hii Maswahabah walimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipowabainishia kwamba kila kitu kinatokana na mipango na makadirio ya Allaah wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Si tutegemee tuliyoandikiwa na tukaacha kufanya matendo?” Akasema: “Hapana; fanyeni matendo. Kwani hakika kila mmoja ni mwenye kuwepesishiwa kile alichoumbiwa.”[3] Ndipo Allaah akateremsha Aayah hii:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa [mali zake] na akamcha Allaah na akasadikisha al-Husnaa, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi.”[4]

Kwa hivyo haijuzu kwa mja kujizuia na kusema ikiwa amekadiriwa kuingia Peponi basi ataingia Peponi na ikiwa amekadiriwa kuingia Motoni basi ataingia Motoni. Jambo hili halijuzu. Mja asiingize jambo hilo katika matendo yake. Je, mtu huketi chini na akaacha kutafuta chakula na kinywaji na akasema kuwa ikiwa Allaah amemkadiria kupata chakula na kinywaji basi atamletea navyo na yeye anakaa chini? Hakuna mwenye kusema hivo. Bali husimama na kutafuta. Akihisi njaa basi husimama na kutafuta chakula na akihisi kiu husimama na kutafuta maji na hasemi kuwa ikiwa Allaah amemkadiria chakula na kinywaji basi atamletea. Kwa sababu maumbile yake yanampelekea kuhangaika na kutafuta.

Akija mtu na kumpiga au akamuua mtoto wake atanyamaza na kusema kuwa haya ni mambo Allaah alikuwa amekwishampangia na kumkadiria au atatafuta kumpiliza? Jibu ni kwamba atatafuta kumlipiza. Ni kwa nini basi hasemi kuwa hayo ni mambo Allaah amempangia na kumkadiria, kutomchukulia hatua muuaji au mpigaji au kuomba kulipiza kisasi? Hii ni dalili inayoonyesha kuwa mambo yana sababu na kwamba mja anatakiwa kufanya sababu na asibaki hivohivo bila kufanya sababu. Allaah amefungamanisha vyenye kusababishwa na sababu zake. Hata ndege na wanyama hawana mtazamo huu. Hawabaki kwenye nyumba zao na kutarajia kujiwa na riziki ilihali wamo ndani ya nyumba zao. Hali ni hivo kwa ndege na wanyama. Wanaruka na kutafuta riziki. Kwa sababu Allaah amewaumba katika maumbile hayo kwamba hawafikii mambo isipokuwa kwa kufanya matendo, kuhangaika na kutafuta:

فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚلَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ

“Imani hiyo ndio maumbile Allaah aliyowaumbia watu [wote] – hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah!”[5]

أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ

“Ambaye amekipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoza.”[6]

 Msemo huu ni wenye kufilisika na uongo. Msemo wenyewe ni kutumia hoja kwa Qadar juu ya kuacha matendo. Muislamu anachotakiwa ni yeye kufanya matendo mema na akifanya dhambi anachotakiwa ni yeye kutubia kwa Allaah. Ana uwezo wa mambo hayo. Anaweza kufanya na anaweza kuacha. Akiacha matendo kwa kushindwa Allaah hatomchukulia hatua. Lakini akiacha kwa uvivu atachukuliwa hatua kwa jambo hilo kwa sababu amezembea. Kuna tofauti kati ya uvivu na kushindwa. Allaah hatomchukulia hatua kwa kushindwa. Lakini atamchukulia hatua kwa uvivu. Kwa sababu yeye ndiye amezembea. Maumbile ya waja yanapelekea hivo pamoja na dalili za Qur-aan na Sunnah.

[1] 92:05-07

[2] 92:08-10

[3] al-Bukhaariy (4945) na Muslim (2647) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] 92:05-07

[5] 30:30

[6] 20:50

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 23/03/2021