Kuhusu wale Maswahabah ambao wameshuhudiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa dhati zao ya kwamba ni katika watu wa Peponi, basi Ahl-ul-Hadiyth wanafanya vivyo hivyo juu yao kwa sababu ya kusadikisha maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ahadi yake kwao. Kwani hakika yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakushuhudia hayo isipokuwa baada ya kuyatambua hayo. Allaah (Ta´ala) alifichulia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale Aliyoyataka katika yaliyofichikana. Dalili ya hilo ni katika maneno Yake (´Azza wa Jall):

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ

”Mjuzi wa mambo yaliyofichikana na wala hamdhihirishii yeyote ghaibu Yake, isipokuwa yule aliyemridhia ambaye ni Mtume.”[1]

Aliwabashiria (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Maswahabah kumi kuingia Peponi, nao ni: Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Twalhah, az-Zubayr, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Sa´d, Sa´iyd na Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah. Vilevile alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Thaabit bin Qays bin Shimaas (Radhiya Allaahu ´anh):

”Hakika ni katika watu wa Peponi.”

Anas bin Maalik amesema:

”Alikuwa anatembea kati yetu na sisi tunasema: ”Hakika yeye ni katika watu wa Peponi.”[2]

[1] 72:26-27

[2] al-Bukhaariy (3613) na Muslim (187).

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 287-289
  • Imechapishwa: 24/12/2023