38. Kisomo cha Qur-aan katika swalah ya usiku

6- Swalah ya usiku

Wakati fulani (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa inatokea anasoma kwa sauti na wakati mwingine anasoma kwa kunyamaza[1]. Mara nyingine akifupisha kisomo na mara nyingine akikirefusha. Wakati mwingine alikuwa anaweza kurefusha kisomo mpaka Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) akasema:

“Usiku mmoja niliswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akarefusha kisimamo mpaka nikaingiwa na mawazo mabaya.” Kukasemwa: “Uliingiwa na nini?” Akasema: “Niliingiwa na kuketi na kumuacha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

Hudhayfah bin al-Yamaan amesema:

“Usiku mmoja niliswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akaianza swalah kwa “al-Baqarah” ambapo nikafikiri kuwa atafanya Rukuu´ baada ya Aayah mia. Akaendelea mbele. Ndipo nikafikiri kuwa atafanya Rukuu´ baada ya Aayah mia mbili. Akaendelea mbele. Ndipo nikafikiri kuwa atarukuu wakati atapoimaliza. Ndipo akawa ameanza “an-Nisaa´” na kuisoma. Halafu akaanza “Aal ´Imraan”[3] na kuisoma. Anasimama katika kila Aayah. Anapofika katika Aayah inayomtakasa Allaah kutokamana na mapungufu, anamtakasa Allaah kutokamana na mapungufu, anapofika katika Aayah ilio na du´aa, huomba du´aa, anapofika katika Aayah inayoomba kinga, huomba kinga. Kisha ndio akaenda Rukuu´… “[4]

Usiku mmoja wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anahisi maumivu alisoma zile Suurah saba ndefu[5].

Wakati mwingine alikuwa anaweza katika kila Rak´ah kusoma Suurah moja katika hizo[6].

Haitambuliki kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipatapo kusoma Qur-aan yote katika usiku mmoja. Bali hakupendelea ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh) afanye hivo wakati alipomwambia:

“Soma Qur-aan yote mara moja kwa mwezi.” Akasema: “Mimi naweza zaidi ya hivyo.” Akasema: “Soma yote kila baada ya nyusiku ishirini.” Akasema: “Mimi naweza zaidi ya hivyo.” Akasema: “Isome yote kila baada ya nyusiku saba na wala usisome zaidi ya hivo.”[7]

Baada ya hapo akamruhusu kuisoma yote kila baada ya siku tano[8] na mwishowe kila baada ya siku tatu[9]. Akamkataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuisoma kwa kasi zaidi ya hiyo[10] na kumweleza sababu:

“Yule atakayesoma Qur-aan [mbiombio] chini ya siku tatu hatoielewa.”[11]

Katika matamshi mengine imekuja:

“Hatoielewa Qur-aan yule mwenye kusoma [mbiombio] chini ya siku tatu.”[12]

Amesema vilevile:

“Kila mja ana shauku[13] na kila shauku ina kipindi ambacho ima ni Sunnah au Bid´ah. Kipindi chake kikimwelekeza katika Sunnah basi ameongoka na kipindi chake kikimwelekeza katika kitu kingine basi ameangamia.”[14]

Kwa ajili hiyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anasoma Qur-aan nzima chini ya siku tatu[15]. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayeswali usiku na kusoma Aayah mia mbili basi huandikwa ni katika watiifu na wakweli.”[16]

Katika kila usiku alisoma Suurah “al-Israa´” na “az-Zumar”[17].

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayeswali usiku na kusoma Aayah moja basi hatoandikwa ni katika waghafilikaji.”[18]

Wakati mwingine hasomi katika kila Rak´ah chini ya Aayah khamsini[19].

Mara nyingine anasoma sawa na kiwango cha “al-Muzammil”[20].

Mara chache mno Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ataswali usiku mzima[21]. ´Abdullaah bin Khabbaab bin al-Arat (ambaye alishuhudia vita vya Badr pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimchunguza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika usiku aliyouswali wote. Mpaka alipomaliza kuswali Fajr akamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Namtoa muhanga baba yangu na mama yangu kwa ajili yako. Leo usiku umeswali swalah ambayo sikuwahi kukuona unaswali mfano wake hapo kabla.” Akasema: “Umesema kweli. Ni swalah ya matumaini na woga. Mimi nimemuomba Mola wangu mambo matatu. Akanipa mambo mawili na ananinyima moja. Nimemuomba Mola wangu asituangamize kama zilivyoangamia nyumati kabla kabla (katika upokezi mwingine imekuja “asiuangamize Ummah wangu kwa sababu ya ukame”), akanipa hilo. Nimemuomba Mola wangu (´Azza wa Jall) asimfanye adui mwenye kutoka nje akaja kutushinda, akanipa hilo. Nimemuomba Mola wangu asitutenganishe makundi kwa makundi, akaninyima hilo.”[22]

Usiku mmoja alikariri Aayah ifuatayo mpaka asubuhi:

إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ ۖ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Ukiwaadhibu basi hao ni waja Wako; na Ukiwasamehe basi hakika Wewe ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[23]

Aliisoma katika Rukuu´ na Sujuud´ na pindi anapoomba du´aa. Kulipopambazuka Abuu Dharr akamwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Umeendelea kusoma Aayah hii mpaka asubuhi ikaingia. Uliisoma katika Rukuu´ na Sujuud na pindi unapoomba du´aa. Kwani Allaah amekufunza Qur-aan yote. Lau mmoja wetu angelifanya hivo tungelimchukulia kwa ubaya.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi nimemuomba Allaah uombezi juu ya Ummah wangu na akanipa. Ataupata kila yule ambaye hamshirikishi Allaah na chochote.”[24]

Mwanamume mmoja akamwambia:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi nina jirani ambaye anaswali usiku na hasomi isipokuwa tu “al-Ikhaasw”. Anaikariri na wala hasomi kitu kingine juu yake.” Kama kwamba mwanamume huyu anaidharau. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake ya kwamba hiyo ni sawa na theluthi ya Qur-aan.”[25]

[1] an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

[3] Imepokelewa namna hii, nako ni ”an-Nisaa´” kabla ya ”Aal ´Imraan”. Ni dalili inayothibitisha ya kwamba inafaa kuacha kusoma kwa mpangilio uliyoko katika Mushaf wa ´Uthmaan.

[4] Muslim na an-Nasaa’iy.

[5] Abu Ya´laa na al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Suurah saba ndefu ni ”al-Baqarah”, ”Aal ´Imraan”, ”an-Nasaa´”, ”al-Maaidah”, ”al-An´aam”, ”al-A´raaf” na ”at-Tawbah”.

[6] Abu Daawuud na an-Nasaa’iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[7] al-Bukhaariy na Muslim.

[8] an-Nasaa’iy na at-Tirmidhiy aliyesema kuwa ni Swahiyh.

[9] al-Bukhaariy na Ahmad.

[10] ad-Daarimiy na Sa´iyd bin Mansuur katika ”as-Sunan” kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[11] Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[12] ad-Daarimiy na at-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa ni Swahiyh.

[13] Imaam at-Twahaawiy amesema:

”Ni hamasa ambayo waislamu wanakuwa nayo katika matendo yao wakati wanapomuabudu Mola wao (´Azza wa Jall). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupenda wawe na hamasa ambayo baadaye hawana budi isipokuwa watakuwa na upungufu na kuachana nayo. Kwa hivyo, badala yake akawaamrisha wafanye matendo mema ambayo wataweza kuyaendeleza siku zote mpaka pale watapokutana na Mola wao (´Azza wa Jall). Imepokelewa ya kwamba amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya maana hii:

“Vitendo vinavyopendwa na Allaah na vile vyenye kudumu japo vitakuwa vichache.”

Hadiyth ambayo amesema kuwa imesimuliwa imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

[14] Ahmad na Ibn Hibbaan ambaye ameisahihisha.

[15] Ibn Sa´d (1/376) na Abuush-Shaykh katika ”Akhlaaq-un-Nabiy (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)” (281).

[16] ad-Daarimiy na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[17] Ahmad na Ibn Naswr kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[18] ad-Daarimiy na al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[19] al-Bukhaariy na Abuu Daawuud.

[20] Ahmad na Abuu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[21] Muslim na Abuu Daawuud. Kutokana na Hadiyth hii imechukizwa kukesha usiku mzima au sehemu kubwa ya usiku na kuswali. Kwa kuwa ni jambo linaenda kinyume na Sunnah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kama ingelikuwa kukesha usiku mzima na kuswali ndio bora, basi lisingelimpita (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani uongofu bora kabisa ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Usidanganyike na kwamba Abuu Haniyfah (Rahimahu Allaah) aliswali Fajr kwa wudhuu´ wa ´ishaa´ kwa miaka arubaini. Kwani haina msingi. ´Allaamah al-Fayruuzaabaadiy amesema:

“Huu ni uongo wa wazi ambao haufai kunasibishwa na imaam. Hakuna fadhila katika hilo. Imaam kama huyu anatakiwa kufanya vyema kuliko hivyo. Bora na kamilifu zaidi ni kutawadha kwa kila swalah. Hili ni kama tutasema kuwa kweli alikuwa akikesha usiku mzima kwa miaka arubaini. Ni jambo linakaribia kutokuwezekana. Hizi ni simulizi kutoka baadhi ya wale washabiki wajinga. Wamesema hivo kuhusu Abu Haniyfah na wengineo. Yote yamezuliwa.” (ar-Radd ´alaal-Mu´taridhw (01/44))

[22] an-Nasaa’iy, Ahmad na at-Twabaraaniy (2/187/1). Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

[23] 5:118

[24] an-Nasaa’iy, Ibn Khuzaymah (1/70/1), Ahmad, Ibn Naswr na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy kaafikiana naye.

[25] Ahmad na al-Bukhaariy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 102-106
  • Imechapishwa: 15/02/2017