38. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya kuonekana Allaah Aakhirah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Kunaingia vilevile katika yale tuliyoyataja kumuamini Allaah, Vitabu Vyake, Malaika Wake na Mitume Wake, ni pamoja na:

Kuamini ya kwamba waumini watamuona siku ya Qiyaamah kwa macho yao kama wanavyoona jua kwenye anga lililo wazi bila ya mawingu, na hali kadhalika kama wauonavyo mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hawatosongamana katika kumuona. Watamuona (Subhaanah) nao watakuwa katika uwanja wa Qiyaamah na kisha watamuona baada ya kuingia Peponi kwa namna Atakayoipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Katika kuamini Siku ya Aakhirah kunaingia:

Kuamini yote aliyoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya yatakayokuwa baada ya mauti. Wanaamini mitihani ya ndani ya kaburi, adhabu ya kaburi na neema zake. Ama mitihani yake, hakika watu watapewa mitihani kwenye makaburi yao. Kila mtu ataulizwa: “Ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Na ni nani Mtume wako?

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

”Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.” (14:27)

Waumini watasema: “Allaah ndio Mola Wangu, Uislamu ndio Dini yangu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume wangu.” Ama wenye mashaka watasema: “Aah! Aah! Sijui. Nilisikia watu wanasema kitu na mimi nikakisema.” Hivyo atapigwa chuma cha Moto na atapiga kelele ya juu kabisa ambayo itasikiwa na viumbe vyote isipokuwa binaadamu. Na lau binaadamu aingeliisikia, basi angelizimia.

Baada ya mtihani huu, kuna ima neema au adhabu mpaka kitaposimama Qiyaamah kikubwa. Roho zitarudishwa miilini. Qiyaamah ambacho Allaah (Ta´ala) Kaelezea katika Kitabu Chake na kupitia ulimi wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakakubaliana juu ya hilo Waislamu, kitasimama. Watu watatoka ndani ya makaburi yao, wakiwa peku, uchi, wasiotahiriwa, wasimame mbele ya Mola wa walimwengu. Jua litajongezwa karibu yao na jasho zao zitafikia vinywa vyao. Mizani itapima na yapimwe matendo ya waja.

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

“Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni wale ambao imekhasirika nafsi zao, [watakuwa] katika [Moto wa] Jahannam ni wenye kudumu.” (23:102-103)

Madaftari yataenezwa ambayo ndani yake kumeandikwa matendo. Kuna ambao watapewa madaftari yao kwa mkono wa kulia, na kuna ambao watapewa madaftari yao kwa mkono wa kushoto au nyuma ya mgongo wao, kama Alivyosema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا

”Na kila mtu Tumemuambatanishia majaaliwa ya ‘amali zake shingoni mwake. Na Tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu atakachokikuta kimekunjuliwa. [Ataambiwa]: “Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosheleze leo kukuhesabia dhidi yako.” (17:13-14)

Allaah Atawafanyia hesabu viumbe na Atamhifadhi mja Wake muumini halafu atayakubali madhambi yake, kama ilivyokuja katika Kitabu na Sunnah. Kuhusu makafiri, hawatohesabiwa hesabu kwa njia hiyo hiyo ya matendo mema na mabaya kupimwa, kwa kuwa hawana mema yoyote. Badala yake matendo yao yatahesabiwa na watakuja kujua hilo, wayakubali na wawajibike nayo.

MAELEZO

Mlango huu unazungumzia juu ya waumini kumuona Mola Wao. Imetangulia kwa sura ya jumla ya kwamba waumini wanaamini yale yote aliyoelezea Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Pepo na Moto, Malaika, madaftari, mizani, kufanyiwa hesabu, malipo na mengineyo kuhusiana na mambo ya Aakhirah. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yote haya kwa njia ya ujumla.

Kunaingia vilevile katika yale tuliyoyataja… – Miongoni mwa hayo vilevile kunaingia kuamini ya kwamba waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah. Haya ni miongoni mwa maelezo kuhusu siku ya Qiyaamah ya kwamba waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah. Amesema (Rahimahu Allaah):

“… kwa macho yao.”

Ina maana ya kwamba watamuona kwa macho yao wazi wazi pasi na kuwepo ugumu wala utata. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hamtosongamana katika kumuona. Vilevile kama mnavyoona jua wazi pasina kuwepo mawingu.”

Makafiri watazuiwa na kumuona Allaah

Kuhusu makafiri hawatomuona. Bali watazuiawa. Amesema (Subhaanah):

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.” (83:15)

Bi maana siku ya Qiyaamah.

Kuhusu waumini watamuona mara mbili:

Mosi: Watamuona kwenye uwanja muono ambao utakuwa ni maalum kwao pasi na wengineo wataokuwa wamesimama uwanjani.

Pili: Watamuona namna anavyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala) Peponi katika nyakati ambazo atawaondoshea pazia ya Uso Wake mtukufu. Peponi watakuwa na nyakati maalum ambazo wanamuona. Kila mmoja atamuona katika nyakati mbali mbali kutegemea na nafasi alionayo.

Katika kuamini Siku ya Aakhirah kunaingia… – Miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah vilevile ni kuamini yale yote aliyoelezea Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ikiwa ni pamoja vilevile na mambo ya Aakhirah, Pepo, Moto, kufanyiwa hesabu na malipo. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yote haya.

Kadhalika inatakiwa kuamini adhabu na neema ya kaburi. Ahl-us-Sunnah wanaamini hayo. Tofauti na Ahl-ul-Bid´ah. Ahl-us-Sunnah wanaamini adhabu na neema ya kaburi, kwamba watu watahojiwa ndani ya makaburi yao ambapo wataulizwa juu ya Mola, dini na Mtume Wao. Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti duniani na Aakhirah na madhalimu huwadhalilisha. Amesema (Subhaanah):

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖوَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo.” (14:27)

Muumini yeye atajibu kwa kusema kwamba Mola Wake ni Allaah, Uislamu ndio dini yake na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume Wake.

Ama yule mwenye shaka na kafiri watasema kuwa hawajui. Hili linahusu mnafiki na kafiri. Huyu ni yule mnafiki ambaye alikuwa akidhihirisha Uislamu ilihali ni kafiri na kafiri wa wazi. Hawa ndio ambao watajibu kusema kuwa hawajui na kwamba walikuwa wakiwasikia watu wakisema kitu na wao wanasema. Atapigwa chuma cha moto na ukelele mkubwa ambao utasikia kila kiumbe isipokuwa mwanaadamu. Lau mwanaadamu angelisikia ukelele huo basi angelizimia.

Baada ya mtihani huu, kuna ima neema au adhabu mpaka kitaposimama Qiyaamah kikubwa… – Baada ya hapo ndipo kutasimama Qiyaamah kikubwa. Haya yatatokea baada ya mtihani [wa ndani ya kaburi ambapo] mwanaadamu huwa ima katika neema au adhabu. Muumini anakuwa katika neema ambapo roho yake inawekwa Peponi. Kafiri roho yake inawekwa Motoni. Amesema (Subhaanah) kuhusu watu wa Fir´awn walioko Motoni:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Wanadhihirishiwa Moto asubuhi na jioni na Siku itakayosimama Qiyaamah [itasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.” (40:46)

Hapa ndipo kitakuwa kimesimama Qiyaamah kikubwa na watu watoke ndani ya makaburi yao peku, uchi na bila ya kutahiriwa. Allaah atawafufua hali ya kuwa amewarudishia miili yao. Watakuwa kama walivyoumbwa mara ya kwanza:

Peku – Bi maana pasi na viatu.

Uchi – Bi manaa hawatokuwa na mavazi.

Wasiotahiriwa – Bi maana watakuwa hawakutahiriwa.

Watasimama kwenda kwa Mola wa walimwengu na Allaah (Jalla wa ´Alaa) atawafanyia hesabu viumbe. Mizani itawekwa na matendo ya waja yapimwe. Yule ambaye mizani yake itakuwa na uzito huyo ndiye mwenye furaha. Ama yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu huyo ndiye mwangamivu.

Madaftari yataenezwa ambayo ndani yake kumeandikwa matendo… – Madaftari yatagawanywa na kusambazwa kati yao. Kuko ambao watapokea madaftari yao kwa mikono ya kulia na wengine watapokea madaftari yao kwa mikono ya kushoto au nyuma ya migongo yao, kama ilivyobainishwa katika Qur-aan.

Kuhusu makafiri, hawatohesabiwa hesabu…Kuhusiana na makafiri hawatofanyiwa hesabu kwa njia ya mema na maovu yao kupimwa. Kwa sababu makafiri hawana mema yoyote. Lakini hata hivyo yatadhibitiwa matendo yao, wayakubali na halafu walipwe kwayo. Kwa msemo mwingine watatupwa Motoni. Matendo yao yatadhibitiwa, wayakubali na wayakiri. Baada ya hapo watupwe Motoni. Amesema (Ta´ala):

وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا

“Na wataendeshwa wale waliokufuru kuelekea [Moto wa] Jahannam makundi-makundi.” (39:71)

Itakuwa ni kundi baada ya kundi. Haya ni kutokamana na matendo yao machafu na kumkufuru kwao Allaah (´Azza wa Jall).

Ama watu wa Peponi wataingizwa Peponi kukirimiwa kikundi baada ya kutoka kwenye kiwanja cha hesabu na baada ya kupita juu ya Njia na kupitia kisimamo kirefu watachosimamishwa. Hapo ndipo sasa wataingizwa Peponi kwa kila mmoja kuwekwa nafasi yake stahiki. Yeye atakuwa anaijua nafasi yake kutokea duniani. Hivyo wataziendea nafasi zao ambazo Allaah amewaandalia baada ya kupitia hatua kadhaa zitatajwa huko mbeleni Allaah akitaka.

Tunachotaka kusema ni kwamba haya ndio mambo ya siku ya Qiyaamah. Ni siku nzito. Siku moja ni sawa na miaka elfu khamsini. Itakuwa ni siku nzito kwa makafiri na nyepesi kwa waumini. Amesema (Ta´ala):

أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُّسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلًا

“Watu wa Jannah Siku hiyo wako katika makazi bora ya kutulia na mahali pazuri kabisa pa kupumzikia.” (25:24)

Watu wa Peponi watakuwa sehemu zao za starehe Peponi na watu wa Motoni watakuwa sehemu zao Motoni.

Hesabu itafanywa na Mola Wako (Jalla wa ´Alaa), ambaye ni al-Hakiym na al-´Adl (Mwenye hekima na Mwadilifu), hadhulumu punje hata kidogo. Amesema (Subhaanah):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah Hadhulumu uzito wa atomu. Na ikiwa ni [‘amali] nzuri Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira mkuu.” (04:40)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah; basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote kile. Na japokuwa ni uzito wa mbegu ya hardali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.” (21:47)

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri [hata kama ni] uzito wa chembe ya atomu basi ataiona, na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ya atomu basi ataiona.” (99:07:08)

Mtu akitoa swadaqah ya pesa moja, tonge moja au tende moja kumpa fakiri inakuwa atomu nyingi na kuwa na uzito mkubwa. Vipi kwa mwenye kutoa mapesa na mapesa na chakula kingi? Bila shaka atalipwa kwayo endapo atakuwa ni mwenye kumtakasia ´ibaadah yake Allaah:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri [hata kama ni] uzito wa chembe ya atomu basi ataiona, na yule atakayetenda shari uzito wa chembe ya atomu basi ataiona.” (99:07:08)

Imepokelewa vilevile kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba alitoa swadaqah ya punje ya zabibu ambapo akaulizwa uzito wake. Akasema:

“Punje hii itakuwa na uzito wa atomu kiasi gani.”[1]

Ninacholenga ni kwamba mtu asidharau swadaqah hata kama itakuwa kidogo. Muhimu atoe kiasi na uwezo wake. Atoe pesa moja, pesa mbili, tonge ya chakula ampe mwombaji, tende moja, tende mbili na kadhalika.

Nimeshatangulia kukuelezeni kisa hichi zaidi ya mara moja ya kwamba kuna mwanamke alikuja kwenye nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuomba akiwa na watoto wawili wakike. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anasema kuwa hawakupata nyumbani isipokuwa tende tatu peke yake. Akachukua zile tende tatu na kumpa yule mwombaji. Yule mwanamke akampa kila msichana tende moja na ile ya tatu akaichukua ili aile yeye. Lakini hata hivyo na ile tende ya tatu akawa amewagawia nayo wale watoto wakike wawili na yeye hakula kitu. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anaelezea kuwa kitendo kile kikamfurahisha. Pindi alipokuja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikamweleza ambapo akasema:

“Hakika Allaah (Subhaanah) amemuwajibishia [mwanamke huyo] Pepo.”[2]

Hili ni kutokana na huruma huu aliokuwa nao juu ya wasichana wake na akawagawia tende zote na yeye hakula kitu. Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa kutoa swadaqah, hata kama itakuwa kwa kitu kidogo, ilimradi mtu ameitoa kwa nia nzuri, ndani yake ina kheri nyingi.

Kilicho muhimu ni mtu atoe swadaqah kwa kile kitachowezekana. Mwenye uwezo wa pesa mia moja, elfu moja, pesa moja, tende moja, tonge ya chakula, nguo na mfano wa haya mtu atoe swadaqah.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.” (64:16)

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah; basi haitodhulumiwa nafsi yoyote ile kitu chochote kile. Na japokuwa ni uzito wa mbegu ya hardali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu.” (21:47)

[1] Ni kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na sio Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh). Ameipokea Ibn ´Abdil-Barr katika “al-Mustadrak” (1881) (08/602).

[2] Muslim (2630) na al-Bukhaariy (1418).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com