37. Inafaa kufupisha na kukusanya kwa ambaye ameenda nyika?

Swali 37: Je, inafaa kwetu kufupisha na kukusanya zile swalah za Rak´ah nne tunapokwenda nyika?

Jibu: Ikiwa maeneo ya nyika mliyokwenda yako mbali na maeneo mnayoishi na kule kwenda kwenu kunazingatiwa kuwa ni safari, basi hapana neno kufupisha ikiwa yale masafa ni takriban 80 km. Kufupisha ndio bora zaidi kuliko kuswali kwa kukamilisha. Hilo ni kwa njia ya kwamba msafiri ataswali Dhuhr Rak´ah mbili, ´Aswr Rak´ah mbili na ´Ishaa Rak´ah mbili. Hapana neno kukusanya kati ya Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Kuacha kukusanya ndio bora ikiwa yule msafiri ni mkazi na amepumzika. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj yake ya kuaga alikuwa akifupisha swalah katika kile kipindi cha kukaa kwake Minaa na wala hakusanyi. Alikusanya ´Arafah na Muzdalifah kwa sababu haja ilipelekea kufanya hivo[1].

Pindi msafiri atapoazimia kukaa mahali kwa zaidi ya siku nne, basi ni lazima kwake kutofupisha. Bali ataswali zile swalah za Rak´ah nne Rak´ah nnenne. Haya ndio maoni ya wanazuoni wengi. Lakini ikiwa ukaaji ni wa siku nne na chini ya hapo, basi kufupisha ndio kutakuwa bora.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/280).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 53-54
  • Imechapishwa: 05/05/2022