al-Bukhaariy ameandika:

“Mlango: Fadhila za anayefiwa na mtoto akatarajia malipo kutoka kwa Allaah na maneno Yake (Ta´ala):

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ

“Wabashirie wenye kusubiri.” 02:155

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Anas aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote katika watu ambaye watoto wake watatu wanakufa kabla ya kubaleghe isipokuwa Allaah atamwingiza Peponi kwa sababu ya huruma Wake mpana kwao.”

Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna waislamu wawili wataofiliwa na watoto watatu kabla ya kubaleghe isipokuwa Allaah atamwingiza Peponi kwa sababu ya huruma Wake mpana kwao. Kutasemwa: “Ingieni Peponi!” Waseme: “Mpaka waje wazazi wetu.” Wataambiwa hivo mara tatu na watajibu hali kadhalika. Wataambiwa: “Ingieni Peponi nyinyi na wazazi wenu!”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia wanawake:

“Hakuna mwanamke yeyote kati yenu atayefiwa na watoto watatu isipokuwa watakuwa ni ngao kwake kutokamana na Moto.” Mwanamke mmoja akasema: “Watoto wawili?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Na wawili.”

Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah aliyesema:

“Kuna mwanamke alikuja na mvulana na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Muombee kwa Allaah! Nimeshazika watatu.” Akasema: “Umeshazika watatu?” Akajibu: “Ndio.” Akasema: “Hakika umejichukulia ngao yenye nguvu kutokamana na Moto.”

Hadiyth hizi zinathibitisha kuwa watoto wa waislamu wako Peponi. Wanachuoni wengi wamenadi maafikiano juu ya hilo. al-Maawardiy amesema:

“Kuhusu watoto wa Mitume kuna maafikiano ya kukata ya kwamba wako Peponi. Kuhusu watoto wa waislamu wengine wote wanachuoni wengi wanaonelea kuwa wako Peponi kwa kukata. Dalili yao ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ

“Wale walioamini na dhuriya yao ikawafuata kwa imani Tutawakutanisha nao dhuriya yao na hatutawapunguzia katika matendo yao chochote.” 52:21

Baadhi ya wasomi wengine wamenyamaza na kusema kuwa hawakatiwi kama ambavyo hawakatiwi wale ambao wana majukumu juu ya matendo yao. Maoni haya ni ya makosa. Mategemeo yao ni Hadiyth Swahiyh ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Alisema wakati mtoto mchanga wa Answaar alipofariki: “Moja katika ndege za Peponi. Hakupatapo kufanya kitendo kiovu na wala hakufikia umri huo.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Au kinyume na hivyo, ee ´Aaishah? Allaah amewaumba watu kwa ajili ya Pepo. Amewaumbia nayo tangu walipokuwa kwenye nyuti za mgongo za baba zao. Amewaumbia vilevile Moto watu. Amewaumbia nao tangu walipokuwa kwenye nyuti za mgongo za baba zao.”

Wanachuoni wameyajibu hayo kwa kusema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkataza ´Aaishah kuharakia kumkatia mtu pasi na kuwa na dalili yenye kukata. an-Nawawiy amesema:

“Kuna uwezekano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyasema haya kabla ya kujua kuwa watoto wa waislamu wataingia Peponi. Alipolijua hayo akasema:

“Hakuna muislamu yeyote katika watu ambaye watoto wake watatu wanakufa kabla ya kubaleghe isipokuwa Allaah atamwingiza Peponi kwa sababu ya huruma Wake mpana kwao.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutaja watoto watatu halafu wawili – na vilevile katika upokezi mtoto mmoja – inaweza kuwa kwamba aliteremshiwa Wahy juu ya hilo wakati anapoulizwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 62-66
  • Imechapishwa: 14/10/2016