Na´y maana yake ni kuwaeleza watu kuhusu kifo cha mtu. Hayo ndio yanafanywa na watu wa zama zetu pindi wanapotangaza kuhusu kifo cha mkubwa au mtu anayejulikana. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema katika “Zaad-ul-Ma´aad”:

“Miongoni mwa uongofu wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa kuacha kutangaza juu ya kifo cha mtu. Bali alikuwa akikataza na kusema: “Ni katika matendo ya kipindi cha kishirikina.”

Haafidhw Dhwiyaa´-ud-Diyn ameandika katika kitabu chake “al-Ahkaam”:

Na´y imechukizwa.”

Kisha akasimulia Hadiyth tatu. Moja wapo ni kutoka kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tahadharini na Na´y. Hakika Na´y ni katika matendo ya kipindi cha kishirikina.”

Ibn Mas´uud amesema:

“Bi maana kutangaza kifo cha maiti.”

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na geni.”

Hudhayfah amesema:

“Ntapokufa basi msitanganze kifo changu. Nachelea isije kuwa Na´y. Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikataza Na´y.”

Ameipokea Imaam Ahmad, Ibn Maajah na at-Tirmidhiy aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri.

Ismaa´iyl bin Ibraahiym amesema:

“Ibn ´Awn alinieleza ya kwamba alimuuliza Ibraahiym: “Na´y imechukizwa?” Akasema: “Ndio. Anapofariki mtu, mtu anapanda juu ya kipando chake na kunadi: “Fulani amekufa.”

Ibn ´Awm amesema tena:

“Nilipokuwa Kuufah nilisikia kuwa Shurayh alikuwa hatangazi Janaazah ya yeyote. Nikamweleza hayo Muhammad bin Siyriyn akasema: “Shurayh anatoka Makkah. Sioni tatizo lolote mtu akamweleza rafiki yake au mkusanyiko wake.”

Ibraahiym amesema:

“Ni sawa mtu kuwaeleza marafiki na wenzake. Kilichochukizwa ni mtu kuyaeneza hayo katika sehemu za hadharani.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna maiti anayekufa walizi wake wakasema: “Bwana wangu!” na mfano wa hayo isipokuwa Allaah huwapa kazi Malaika wawili kumsukuma kifuani mwake na kumwambia: “Ni kweli ulikuwa hivo?”

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na geni.”

Hadiyth hizi zinathibitisha kuwa kitendo hicho kimekatazwa na kwamba ni katika matendo ya kipindi cha kishirikina. Baadhi ya Hadiyth tulizotaja zinaonyesha kwamba Na´y ni kutangaza juu ya kifo cha mtu fulani na zingine zinaonyesha kuwa ni kutaja zile sifa nzuri za maiti. Udhahiri ni kwamba yote mawili ni Na´y na Allaah ndiye mwenye kujua zaidi. Yale yanayofanywa na baadhi ya watu wa leo ambapo wanawatangazia watu hadharani juu ya kifo cha mtu ni Bid´ah inayokatazwa. Isitoshe inapelekea mchakato wa mazishi kucheleweshwa sana ili wakusanyike na kuachwa Sunnah ya kuharakisha kuzika. Imethibiti katika “as-Sunan” ya Abu Daawuud ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwendea Abu Twalhah bin al-Baraa´ pindi alipokuwa mgonjwa na kumwambia:

“Naona kuwa Twalhah yuko katika kukata roho. Nielezeni juu yake na mfanye haraka. Haitakiwi jeneza la muislamu kukwama kwa familia yake.”

Hata hivyo inafaa kutaja zile sifa nzuri za maiti ikiwa inahusiana tu na maneno mepesi tu na madogo kwa sharti hayo yanayosemwa iwe ni kweli na isiwe kwa njia ya kuomboleza na ya hasira. Katika hali hii sio haramu na wala hayapingani na subira. Imaam Ahmad amesema kuwa maneno mepesi, madogo na ya kweli hayapingani na ile subira ya wajibu. Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) aliingia kwake, akambusu kwenye paji la uso na kusema:

“Mtume wangu! Rafiki yangu wa karibu! Mteuliwa wangu!”

Ameipokea Ahmad.

Vilevile Abu Hurayrah ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangaza kuhusu kifo cha an-Najaashiy siku ile ile aliyokufa. Akawachukua kwenda sehemu ya kuswalia, akawapangisha safu na akampigia Takbiyr nne. Haya yamepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim. Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mtakieni msamaha ndugu yenu!”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 14/10/2016