36. Unawanasihi nini vijana walioacha darsa za wanazuoni na kwenda katika mihadhara ya kisasa?

Swali 36: Wako vijana ambao wanaacha kufuatilia darsa zilizorekodiwa na darsa za wanazuoni wanaoaminika kwa sababu wanaziona kuwa sio muhimu au manufaa yake ni machache. Badala yake wameelekea mihadhara ya kileo ambayo inazungumzia siasa na hali za ulimwenguni kwa sababu wanaona kuwa ndio muhimu zaidi kwa sababu inatilia mkazo mambo ya kisasa. Kipi unachowanasihi mfano wa vijana hawa?

Jibu: Kujishughulisha na mihadhara ya jumla, vyombo vya mawasiliano na yale yanayoendelea ulimwenguni pasi na kuwa na utambuzi juu ya ´Aqiydah na Shari´ah ni upotofu na kupotea. Mtu kama huyo atakuwa ni mwenye kuchanganyikiwa katika fikira kwa sababu amekiacha kilicho bora kwa kilicho kibaya. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametuamrisha kwanza kujifunza elimu yenye manufaa. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi tambua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na [omba msamaha] kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike!”[1]

قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua? Hakika wanakumbuka wenye akili tu.”[2]

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika si venginevo wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[3]

وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا

“Sema: ”Mola wangu! Nizidishie elimu.”[4]

Kuna Aayah nyenginezo kama hizo zinazohamasisha kutafuta elimu iliyoteremshwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Elimu hiyo ndio yenye manufaa inayonufaisha duniani na Aakhirah. Elimu hiyo ndio nuru inayomwangazia mtu njia ya kuelekea Peponi na katika furaha; maisha mazuri na masafi duniani na furaha Aakhirah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَكُم بُرْهَانٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَأَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ نُورًا مُّبِينًا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَاعْتَصَمُوا بِهِ فَسَيُدْخِلُهُمْ فِي رَحْمَةٍ مِّنْهُ وَفَضْلٍ وَيَهْدِيهِمْ إِلَيْهِ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا

”Enyi watu! Kwa hakika zimekujieni hoja kutoka kwa Mola wenu na tumekuteremshieni nuru ya wazi. Ama wale waliomuamini Allaah na wakashikamana Naye, basi hao atawaingiza katika rehema itokayo Kwake na fadhilah na atawaongoza njia iliyonyooka kuelekea Kwake.”[5]

Katika kila Rak´ah tunasoma Suurah ”al-Faatihah” na ndani yake kuna du´aa tukufu:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea!”[6]

Wale ambao Allaah amewaneemesha ni wale ambao wamekusanya kati ya elimu yenye manufaa na matendo mema:

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[7]

غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ

”… si ya walioghadhibikiwa… ”

Hawa ni wale ambao hawaitendei kazi elimu yao:

وَلَا الضَّالِّينَ

”… wala waliopotea!”

Ni wale wanaofanya matendo pasi na elimu.

Kundi la kwanza limeghadhibikiwa na Allaah kwa sababu wamemuasi Allaah kutokana na utambuzi.

Kundi la pili ni potofu kwa sababu wamefanya matendo pasi na elimu.

Hakuna wanaookoka isipokuwa wale ambao Allaah amewaneemesha; ni wale walio na elimu yenye manufaa na matendo mema. Kwa hiyo ni lazima tuyaweke hayo akilini mwetu.

Kuhusu kujishughulisha na hali za kisasa, kama wanavosema ”Fiqh-ul-Waaqiy´”, hayo yanakuwa baada ya kuitambua Shari´ah. Kwa vile anayetambua Shari´ah hutazama mambo ya kisasa na yale yanayopitika ulimwenguni na zile fikira na maoni yanayokuwemo humo. Baada ya hapo anazisoma kwa mujibu wa elimu ya Shari´ah na iliyo sahihi ili aweze kupambanua kati ya kheri na shari. Pasi na elimu ya Shari´ah mtu hawezi kupambanua kati ya haki, batili, uongofu na upotevu[8]. Ambaye hana elimu juu ya dini yake na anajishughulisha na mambo ya elimu kwa jumla, vyombo vya mawasiliano na mambo ya kisiasa hupotea kwa mambo haya. Kwa sababu yote hayo yaliyotajwa hapo juu kwa kiasi kikubwa yana upotofu, madai ya batili na udanganyifu.

[1] 47:19

[2] 39:9

[3] 35:28

[4] 20:114

[5] 4:174-175

[6] 1:6-7

[7] 4:69

[8] Watu wanaojishugulisha na ile wanayoita ”Fiqh-ul-Waaqiy´” limefichuka jambo lao wakati wa vita vya Ghuba pindi walipopingana na fatwa ya Kibaar-ul-´Ulamaa na wakadhani kuwa papara zao zitazaa matunda na kuwa elimu na fikira zao za kisiasa zitashinda. Lakini mambo hayakuwa hivo!

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 97-99
  • Imechapishwa: 25/02/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy