35. Vitabu gani vinatakiwa kusomwa na vinasomwa kutoka kwa kina nani?

Swali 35: Baadhi ya vijana wanavipa mgongo vitabu vya Salaf ambavyo vinasahihisha ´Aqiydah kama vile ”Kitaab-us-Sunnah” cha Ibn Abiy ´Aaswim ambacho kinaweka wazi mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na msimamo wa Sunnah na Ahl-us-Sunnah pamoja na Bid´ah na Ahl-ul-Bid´ah. Badala yake wanajishughulisha kusoma vitabu vilivyoandikwa na wale wanaoitwa wafikiriaji na walinganizi ambao katika maneno yao kuna mambo yanayopingana na vitabu vya Salaf. Ni kipi unachowanasihi vijana hawa? Ni vitabu vyepi vya Salafiyyah ambavyo unapendekeza wavisome?

Jibu: Wakati tulipojua kuwa ni lazima kuitilia umuhimu na kujifunza ´Aqiydah kuna swali linalofuata ”Tunatakiwa kujifunza ´Aqiydah kutoka wapi?” na ”Ni kina nani ambao tutajifunza kutoka kwao ´Aqiydah hii?”

Vyanzo ambavyo kunachukuliwa ´Aqiydah na imani ni Qur-aan, Sunnah na mfumo wa Salaf. Hakika Qur-aan imeibainisha ´Aqiydah ubainifu wa kutosheleza na imebainisha yale yanayoenda kinyume nayo, yale yanayopingana nayo na yale yanayoitia kasoro[1]. Imeyapima maradhi yote yanayoitia kasoro. Vivyo hivyo Sunnah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), maisha yake, ulinganizi wake na Hadiyth zake[2]. Hali kadhalika Salaf[3]; Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wanafunzi wa wanafunzi wa Maswahabah. Hivi ndivo vizazi vyema. Walitilia umuhimu kuifasiri Qur-aan, kuipambanua Sunnah na kuibainisha ´Aqiydah sahihi na kuwafikishia nayo watu. Baada ya Qur-aan na Sunnah inatakiwa kurejea katika maneno ya Salaf ambayo yamehifadhiwa katika vitabu vinavyoifasiri na kuipambanua Qur-aan na Sunnah. Aidha imeandikwa katika vitabu vya ´Aqiydah.

Kuhusu ambao ´Aqiydah inatakiwa kusomwa kutoka kwao, ni wale watu wa Tawhiyd na wanazuoni wa Tawhiyd ambao wameisoma ´Aqiydah hii kwa ndani kabisa na wakaielewa. Nao ni wengi na khaswa katika nchi hii inayotendea kazi Tawhiyd[4]. Hakika wanazuoni wote kwa njia ya ujumla na khaswa wanazuoni wa nchi hii wanatilia umuhimu somo la ´Aqiydah. Wanaisoma na kuifahamu na kuwabainishia nayo watu na kuwalingania kwayo. Kujifunza somo la Tawhiyd wanatakiwa kurejelewa watu na wanazuoni wanaoifanyia kazi Tawhiyd ambao imesalimika na kutakasika ´Aqiydah yao.

Ama kuipuuza ´Aqiydah na kwenda katika vitabu vya elimu za jumla na fikira zinazotoka nje ni jambo lisilonufaisha kitu. Haidhuru kuwa mjinga juu ya vitabu hivi na wala hainufaishi kuvitambua[5]. Lakini ikiwa mtu ameisoma Tawhiyd, ´Aqiydah na elimu nyenginezo za Shari´ah vya kutosha na akataka kuvisoma ili kujua neema ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amemtunuku kwa njia ya ´Aqiydah sahihi ambayo watu hawa wameikosa kwa sababu ya kujishughulisha na porojo na maneno ya kwenye vitabu na magazeti yasiyokuwa na faida yoyote na ambavyo shari yake ni kubwa zaidi kuliko kheri yake, basi hapana neno kwa sharti visimshughulishe mtu na kusoma mambo yaliyo na manufaa kwake. Haijuzu kwa mwanafunzi, khaswa yule mwanafunzi anayeanza, kujishughulisha na vitabu hivi. Kwa sababu havinufaishi na vinapoteza muda na kufanya fikira za msomaji kuparanganya na kupoteza wakati wa mtu.

Kwa hivyo ni wajibu kwa mtu kuchagua vitabu vyenye manufaa na vitabu vyenye faida vinavyoitilia umuhimu Qur-aan na Sunnah na kupambanua ufahamu wa Salaf. Elimu inahusiana na yale aliyosema Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Elimi ni yale aliyosema Allaah, aliyosema Mtume Wake na waliyosema Maswahabah

wao ndio wanazuoni

Elimu si kujiteua mwenyewe kijinga

katika tofauti kati ya Maandiko na maoni ya fulani[6]

[1] Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا بَيْنَ ذَٰلِكَ ۚ وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا

”Na yaliyoko kati ya hayo; na Mola wako si Mwenye Kusahau kamwe.” (19:64)

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

[2] Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mimi nimekuachieni yale ambayo endapo mtashikamana nayo basi hamtopotea; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”  (al-Haakim (1/93))

[3] ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Fuateni na wala msizue. Kwani mmetoshelezwa.” (as-Sunnah (28) ya Ibn Naswr na as-Sunan (1/80) ya ad-Daarimiy)

[4] Saudi Arabia.

[5] Ee Allaah! Tuzidishie ujinga juu yavyo na utuzidishie utambuzi juu ya Tawhiyd!

[6] Kutoka katika mashairi ya Imaam Shams-ud-Diyn bin Qayyim-il-Jawziyyah ”an-Nuuniyyah”.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 94-97
  • Imechapishwa: 16/02/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy