Swali 34: Katika hichi kipindi cha mwisho wako baadhi ya vijana wanaoonekana kupuuza kujifunza mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na badala yake wanajishughulisha na mambo mengine. Unawanasihi nini vijana kama hao?

Jibu: Mimi nawanasihi vijana na waislamu wengine kwanza waitilie umuhimu ´Aqiydah[1]. ´Aqiydah ndio msingi ambao kunajengwa juu yake matendo mengine yote ima kukubaliwa au kukataliwa kwake. Pale ambapo ´Aqiydah inakuwa sahihi na yenye kuafikiana na yale yaliyokuja kutoka kwa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na khaswa Mtume wa mwisho, ambaye ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi matendo mengine yatakubaliwa muda wa kuwa yamefanywa kwa ajili ya Allaah pekee na ni yenye kuafikiana na yale Allaah na Mtume wameyaweka katika Shari´ah. Na ´Aqiydah ikiwa mbovu au potofu, iliyojengeka juu ya desturi na ada za mababu au ´Aqiydah ikawa ya kishirikina, basi matendo hayo ni yenye kurudishwa na hayakubaliwi ijapowa mwenye nayo ameyafanya kwa ajili ya Allaah pekee. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hayakubali matendo yoyote isipokuwa yale yaliyofanywa kwa ajili Yake pekee na kwa mujibu wa Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Yule anayetaka kuikoa nafsi yake, matendo yake yakubaliwe na awe muislamu wa haki, basi aitilie umuhimu ´Aqiydah. Anapaswa kuitambua ´Aqiydah sahihi na yanayopingana nayo na yanayoichengua ili aweze kuyajenga matendo yake juu yake. Hilo halipatikani isipokuwa kwa kujifunza nayo kutoka kwa wanazuoni ambao wameisoma kutoka kwa Salaf[2] wa ummah huu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi tambua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na [omba msamaha] kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike!”[3]

al-Bukhaariy ameandika kichwa cha khabari ”Elimu kabla ya maneno na matendo”[4] na akaitaja Aayah hii iliyotajwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanadamu bila shaka yumo katika khasara, isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa haki na wakausiana subira.”[5]

Ametaja mambo manne ndio ambayo yanamwokoa mtu kutokana na maangamivu:

1 – Imani, kukimaanishwa ´Aqiydah sahihi.

2 – Matendo na maneno mema. Ingawa matendo ni sehemu ya imani Ameyataja kwa kuyatenganisha ili kusisitiza umuhimu wake.

3 – Kuusiana kwa haki. Kwa msemo mwingine kulingania kwa Allaah, kuamrisha mema na kukataza maovu.

4 – Kuusiana kuwa na subira juu ya zile shida na matatizo yanayomkuta mtu katika njia hiyo.

Hakuna mafanikio kwa muislamu isipokuwa akihakikisha mambo haya manne. Kuhusu kutilia umuhimu elimu za jumla, kusoma magazeti na kutafiti yanayoendelea ulimwenguni, haya mtu huyarejelea baada ya kuihakiki Tawhiyd na ´Aqiydah. Hapo ndipo mtu atayaangalia haya ili aweze kupambanua kheri kutokana na shari na kwa ajili ajihadhari kutokana na yale yanayoendelea ulimwenguni katika shari na propapanga zinazopotosha. Lakini ni baada ya kujipamba na elimu juu ya kumwamini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hainufaishi kitu kusoma majarida, magazeti na mambo ya siasa ilihali mtu hana utambuzi wa ´Aqiydah na utambuzi wa dini. Huyu anajishughulisha na mambo yasiyokuwa na faida naye na wala hayawezi kumfanya kupambanua kati ya haki na batili. Wengi ambao hawajui ´Aqiydah na wakatilia umuhimu mambo haya wamepotea wao na wakawapotosha wengine. Wamewatia watu mchanga wa machoni[6] kwa sababu hawana utambuzi na hawana elimu inayoweza kuwafanya kuweza kupambanua kati ya yanayonufaisha na yanayodhuru, yanayotakikana kuchukuliwa na yanayotakikana kuachwa na mambo yanatakiwa kutatuliwa vipi. Kwa ajili hiyo wengi wao wamefikwa na kasoro na mkanganyiko kwa sababu wameingilia mambo ya magazeti na kujishughulisha na mambo ya siasa pasi na kuwa na elimu juu ya ´Aqiydah na dini. Matokeo yake wakaiona haki kuwa ndio batili na batili kuwa ndio haki.

[1] Shaykh wetu amejenga mfumo huu juu ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yaliyopokelewa na Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anh):

”Dini ni kupeana nasaha.” Tukasema: ”Kwa nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Kwa Allaah, Kitabu Chake, Mtume Wake, viongozi wa waislamu na watu wao wa kawaida.” (Muslim (55))

na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomtuma kwenda Yemen:

”Iwe jambo la kwanza utakalowalingania kwalo ni hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.” (al-Bukhaariy (6937))

[2] Vilevile anatakiwa awe miongoni mwa wale ambao wanazuoni wanaowatakia watu wema wamewapendekeza kuwa ni waongofu, nia safi na elimu yenye kubobea.  Wasiwe ni miongoni mwa watu wa Ahl-ul-Ahwaa´ wa vyamavyama na mapote potofu.

[3] 47:19

[4] al-Bukhaariy (1/37).

[5] 103:1-4

[6] Namna hi ndivo wanavofanya wanaharakati wa siasa na Hizbiyuun ambao wanazishugulisha jamii za Kiislamu huku na kule kuwa na mihemko ya kisiasa katika mihadhara, Khutbah, makala na vitabu vyao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 91-94
  • Imechapishwa: 25/02/2024