Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo ya tatu ni kusoma “al-Faatihah” nayo ni nguzo katika kila Rak´ah. Kama ilivyo katika Hadiyth:

“Hana swalah kwa yule asiyesoma ufunguzi wa kitabu.”

Nayo ndiyo mama wa Qur-aan.

MAELEZO

Maneno yake mtunzi:

”Nguzo ya pili ni kusoma “al-Faatihah.”

Ni Aayah saba. Maneno yake mtunzi:

“Nayo ni nguzo katika kila Rak´ah.”

Ni nguzo juu ya imamu na ambaye anaswali peke yake. Haidondoki; si kwa kusahau, kwa kukusudia wala kwa ujinga.

Ni lazima kwa imamu aisome. Endapo ataiacha basi swalah yake inabatilika. Iwapo hatoisoma katika Rak´ah miongoni mwa Rak´ah basi Rak´ah hii itabatilika na itampasa kuleta Rak´ah nyingine badala yake. Vivyo hivyo juu ya ambaye anaswali peke yake.

Kuhusu maamuma akisoma al-Faatihah juu yake ni wajibu uliowepesishwa. Inamdondokea pale anapoingia ndani ya swalah akamkuta imamu yuko katika Rukuu´. Amepokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba alijiunga na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati ambapo alikuwa amerukuu ambapo akarukuu kabla ya kufika katika safu. Akamtajia kitendo hicho Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema:

“Allaah akuzidishie pupa na wala usirudie tena.”[1]

Lakini hakumwamrisha kuswali upya Rak´ah nyingine.

Kadhalika akija na hakukubaki katika kisimamo isipokuwa kiwango kidogo ambacho hakitoshelezi kusoma al-Faatihah. Vilevile akiigiliza yale maoni ya wale wenye kuona kuwa sio lazima[2]. Hali kadhalika akisahau. Kusoma al-Faatihah juu ya haki ya maamuma ni haki iliyowepesishwa. Kwa msemo mwingine inadondoka wakati wa kusahau, wakati wa kuigiliza au akija na kumkuta imamu yuko kwenye Rukuu´.

Maneno yake:

Kama ilivyo katika Hadiyth:

“Hana swalah kwa yule asiyesoma ufunguzi wa kitabu.”

Imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim[3] kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh).

Maneno yake:

“Nayo ndiyo mama wa Qur-aan.”

Kama ilivyo katika tamko la Muslim kupitia kwa ´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh). Imeitwa “mama wa Qur-aan” kwa sababu maana nzima ya Qur-aan ni yenye kurejea kwayo.

[1] al-Bukhaariy (783).

[2] Tazama ”al-Mughniy” (01/283).

[3] al-Bukhaariy (756) na Muslim (394).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 13/06/2022