36. Kupinga kwa Jahmiyyah kuwa Allaah alimzugumzisha Muusa maneno ya kweli

Tuliwauliza ni kwa nini wamepinga jambo hilo. Wakajibu kuwa Allaah hakuzungumza na wala hazungumzi. Badala yake wanadai kuwa Allaah (´Azza wa Jall) aliumba kitu ambacho kikazungumza kwa niaba yake; akaumba sauti yenye kusikika. Wanadai kuwa maneno hayawi isipokuwa kwa kitu kilicho na tundu, mdomo, midomo na ulimi.  Tukawauliza kama inafaa kwa kiumbe, au mwengine asiyekuwa Allaah, kusema kumwambia Muusa:

إِنِّي أَنَا رَبُّكَ فَاخْلَعْ نَعْلَيْكَ ۖ إِنَّكَ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى

”Hakika mimi ni Mola wako! Hivyo vua viatu vyako; hakika wewe uko katika bonde takatifu la Twuwaa.”[1]

إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي

”Hakika mimi ni Allaah, hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi, hivyo basi niabudu na simamisha swalah kwa ajili ya kunitaja!”[2]

Yule mwenye kudai hivo, basi amedai kuwa kuna mwengine asiyekuwa Allaah ambaye amedai Uola. Mambo yangelikuwa kama anavodai al-Jahm ya kwamba Allaah ameumba kiumbe kama hicho, basi ina maana kuwa kiumbe hicho kilisema:

يَا مُوسَىٰ إِنِّي أَنَا اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Ee Muusa! Hakika Mimi ni Allaah, Mola wa walimwengu!”[3]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا

”Na bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno kihakika.”[4]

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ

“Na alipokuja Muusa katika miadi Yetu na Mola wake akamsemesha.”[5]

يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي

”Ee Muusa! Hakika Mimi nimekuteua juu ya watu kwa Ujumbe na maneno Yangu.”[6]

Haya yote yako ndani ya Qur-aan.

Kusema kwao kuwa Allaah hazungumzi basi mtu anaweza kujiuliza ni upi msimamo walioshika juu ya Athar aliyosimulia al-A´mash, kutoka kwa Khaythamah, kutoka kwa ´Adiyy bin Haatim at-Twaa’iy, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna yeyote katika nyinyi isipokuwa atazungumza na Mola wake pasi na kati yao kuwepo na mkalimani.”[7]

Kuhusu madai yao kwamba maneno hayawi isipokuwa kutoka katika kitu kilicho na tundu, mdomo, midomo na ulimi. Allaah si amesema kuziambia mbingu na ardhi:

ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ

”Njooni kwa kutaka au kwa lazima!” – zikasema: ”Tumekuja hali ya kuwa tumetii!” [8]?

Je, waona kuwa vimezungumza hivo kwa tundu, mdomo, midomo, ulimi na nyenzo nyingine? Amesema tena (Ta´ala):

وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ ۚ وَكُنَّا فَاعِلِينَ

”Tukatiisha majibali iwe pamoja na Daawuud ikatukuza pamoja na ndege – na Sisi tulikuwa ni wenye kuyafanya hayo.”[9]

Je, unaona kuwa vitazungumza kwa tundu, mdomo, ulimi na midomo?

Wakati viungo vitapotoa ushuhuda dhidi ya makafiri, makafiri watasema:

لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ

”Mbona mnashuhudia dhidi yetu?” – zitasema: ”Ametutamkisha Allaah, ambaye amekitamkisha kila kitu.”[10]

Je, unaona kuwa vitazungumza kwa tundu, midomo na ndimi? Walisema hivo kwa tundu na kwa kuwepa midomo na ndimi? Uhakika wa mambo ni kwamba Allaah ndiye ambaye anavitamkisha anavotaka. Vivyo hivyo Allaah anazungumza anavotaka pasi na tundu, mdomo, midomo na ulimi[11].

[1] 20:11-12

[2] 20:14

[3] 28:30

[4] 4:164

[5] 7:143

[6] 7:144

[7] al-Bukhaariy (6539) na Muslim (1016).

[8] 41:11

[9] 21:79

[10] 41:21

[11] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 135-137
  • Imechapishwa: 24/04/2024