Tuliwauliza ni kwa nini wanapinga kuwa wakazi wa Peponi wtamuona Mola wao. Wakajibu kwamba haitakikani kwa yeyote kumuona Mola wake, kwa sababu anayeangaliwa anajulikana na ameelezwa. Hakuna kinachoonekana isipokuwa kitendo Chake. Tukasema si ni Allaah ndiye anasema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَى رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitang´ara – zikimtazama Mola wao.”

Wakasema kuwa Aayah (إِلَى رَبِّهَا نَاظِرَةٌ) maana yake ni kwamba wanatazama malipo ya Mola wake. Watachoangalia ni kitendo na uwezo Wake. Wakajengea hoja kwa Aayah isemayo:

أَلَمْ تَرَ إِلَىٰ رَبِّكَ كَيْفَ مَدَّ الظِّلَّ

”Je, huoni namna Mola wako alivyotandaza kivuli?”[1]

Wakasema, maana yake, huoni kitendo cha Mola wako? Ndipo tukasema kuwa mja daima ni mwenye kuona matendo ya Allaah, lakini hapa anasema:

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote.”[2]

Wakasema, maana yake, ni kwamba wanasubiri malipo kutoka kwa Mola wake. Ndipo tukasema kuwa watamuona Mola wao wakati wanasubiri malipo yao.

Wakasema tena kuwa Allaah haonekani duniani wala Aakhirah. Wakatumia hoja kwa Aayah zisizokuwa wazi, ikiwa ni pamoja na maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye alikuwa anajua maana ya Aayah hiyo, amesema:

”Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu.”[3]

Amesema (´Azza wa Jall) kumwambia Muusa (´alayhis-Salaam):

لَن تَرَانِي

“Hutoniona.”[4]

Hakusema kuwa Yeye haonekani.

Ni maneno ya nani yana haki kufuatwa; maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema ”Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu” au maneno ya Jahmiyyah, wanaosema kuwa hatutomuona Mola wetu? Hadiyth zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zilizoko kwa wanazuoni zinasema kuwa wakazi wa Peponi watamuona Mola wao. Hakuna wanazuoni wanaotofautiana juu ya hilo.

Sufyaan amesimulia kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa ´Aamir bin Sa´d, ambaye amesema kuhusu maneno ya Allaah (Ta´ala):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.”[5]

”Kuangalia uso wa Allaah.”

Thaabit al-Bunaaniy amesimulia kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa, kutoka kwa Suhayb, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Watapothibiti wakazi wa Peponi Peponi, basi ataita kwa sauti mwenye kuita: ”Enyi wakazi wa Peponi! Hakika Allaah amekupeni ruhusa ya ziada.” Ndipo afunue pazia na Ajidhihirishe kwao.”[6]

Wamuone Allaah – hapana mungu wa haki mwingine asiyekuwa Yeye. Tunataraji ya kuwa al-Jahm na wafuasi wake hawatokuwa miongoni mwa wale watakaomuona Mola wao na watazuiwa kutokana Naye. Kwa sababu Allaah amesema kuhusu makafiri:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.”[7]

Ikiwa kafiri atazuiwa kutokana na Allaah na muumini atazuiwa kutokana na Allaah, ni upi basi ubora alionao muumini juu ya kafiri? Himdi zote njema ni stahiki Yake Allaah ambaye hakutufanya kuwa kama al-Jahm na wafuasi wake, na Akatufanya kuwa katika wale wanaofata na si katika wale wanaozua. Himdi zote njema ni Zake pekee[8].

[1] 25:45

[2] 6:103

[3] al-Bukhaariy (554) na Muslim (633).

[4] 7:143

[5] 10:26

[6] Ahmad (4/332), Muslim (181), at-Tirmidhiy (2552) na (3105) na Ibn Maajah (187).

[7] 83:15

[8] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 129-134
  • Imechapishwa: 24/04/2024