Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Haya na yanayofanana na haya katika yaliyothibiti mlolongo wa wapokezi wake na wapokezi wake wamekubaliwa, tunayaamini na wala hatuyarudishi na wala hatuyakanushi na wala hatuyafasiri kwa maana yenye kwenda kinyume na udhahiri wake. Aidha hatuyashabihishi na sifa za viumbe na kwa maneno ya wenye kuzua. Tunajua ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hana yeyote anayeshabihiana na kulingana Naye:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

”Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Kwa hakika Allaah ni tofauti kabisa na yote yanayomjia mtu akilini na kwenye fikira zake. Miongoni mwa hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[2]

MAELEZO

13 – Kulingana juu ya ´Arshi. Kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi ni miongoni mwa sifa za Allaah zilizomthubutikia kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf. Allaah (Ta´ala) amesema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah alipomaliza [kuumba] viumbe aliandika huko Kwake juu ya ´Arshi “Hakika rehema Zangu zinashinda ghadhabu Zangu.””[3]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Abu Daawuud amepokea katika “Sunan” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umbali uliopo kati ya mbingu moja hadi nyingine ni ima mwaka mmoja, miwili au mitatu au miaka sabini na tatu… “ mpaka alipofikia kusema: “…baina ya chini ya ´Arshi na juu yake ni kama mfano wa mbingu hadi mbingu nyingine kisha Allaah (Ta´ala) yuko juu ya yote hayo.”

Ameipokea pia at-Tirmidhiy na Ibn Maajah. Ndani yake kuna kasoro ambayo imejibiwa na Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika “Tahdhiyb Sunan Abiy Daawuud, ukurasa wa 27, 92, 93 juzu ya 07.

Salaf wameafikiana juu ya kumthibitishia Allaah kulingana juu ya ´Arshi Yake. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo pasi na kupotosha, kukanusha, kuifanyia namna wala kuipigia mfano. Ni kulingana kikweli. Maana yake ni kuwa juu, kuthibiti na kutulia kwa njia inayolingana na Allaah.

Ahl-ut-Ta´twiyl wameifasiri eti ni kutawala. Tunawaraddi kwa yale yaliyokwishatangulia katika kanuni ya nne. Tunazidisha njia ya nne ambayo ni kwamba maana hiyo haitambuliki katika lugha ya kiarabu. Aidha njia ya  tano ni kuwa inapelekea katika malazimisho batili kwa mfano ya kwamba hakuwa mwenye kumiliki ´Arshi kisha baadaye ndipo akaitawala.

´Arshi maana yake kwa mujibu wa lugha ni kiti maalum cha mfalme.

´Arshi kwa mujibu wa Shari´ah ni ´Arshi tukufu ambayo Allaah (Jalla Jallaaluh) amelingana juu yake. Ndio kiumbe kilicho juu na kikubwa zaidi. Allaah amekisifu kuwa ni kikuu, karimu na kitukufu.

Kursiy ni tofauti na ´Arshi. ´Arshi ni kile ambacho Allaah (Ta´ala) amelingana juu yake. Kursiy ni mahali pa kuwekea miguu. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Kursiy ni mahali pa kuwekea miguu na ´Arshi hakuna yeyote awezaye kukisia ukubwa wake.”

Ameipokea al-Haakim katika “al-Mustadrak” yake na akasema kuwa ni Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim lakini hawakuipokea[4].

[1] 42:11

[2] 20:05

[3] al-Bukhaariy (7554) na Muslim (2751).

[4] al-Haakim (02/282).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 61-64
  • Imechapishwa: 26/10/2022