Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala):

أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ

”Je, mnajiaminisha na Yule Aliyeko mbinguni.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola Wetu ni Allaah Aliye juu ya mbingu, limetakasika jina Lako.”[2]

Alimwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mjakazi: “Allaah yuko wapi?” Akasema: “Juu ya mbingu.” Hivyo akasema: “Mwache huru, kwani hakika ni muumini.”[3]

Ameipokea Maalik bin Anas, Muslim na maimamu wengine.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia Huswayn:

“Unaabudu waungu wangapi?” Akasema: “Saba, sita wako katika ardhi na mmoja Yuko juu mbinguni.” Mtume akamuuliza: “Ni nani unayemwendea wakati wa matumaini na wakati wa khofu?” Huswayn akasema: “Ni Yule ambaye yuko mbinguni.” Mtume akamwambia: “Waache hao sita na mwabudu Yule Aliye mbinguni, na mimi nitakufunza du´aa mbili.” Akaingia katika Uislamu na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamfunza aseme:

اللهم ألهمني رشدي، وقني شر نفسي

“Eeh Allaah niongoze katika uongofu na nikinge na shari ya nafsi yangu.”[4]

Hali kadhalika katika mambo yaliyopokelewa katika vitabu vya kale, ni kwamba alama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake ni kuwa wanasujudu katika ardhi na wanadai kuwa mungu wao yuko mbinguni. Abu Daawuud amepokea katika “as-Sunan” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kwa hakika umbali wa kati ya mbingu hadi mbingu nyingine ni mwendo wa kadhaa na kadhaa… “ akaendelea kuelezea mpaka alipofikia kusema: “Juu ya hayo kuna ´Arshi na Allaah (Subhaanah) Yuko juu yake.”[5]

Haya na yanayofanana na haya Salaf (Rahimahumu Allaah) wameafikiana kwayo na wameyanukuu na kuyakubali. Hakuna aliyethubutu kuyarudisha, kuyapindisha maana, kuyashabihisha na kuyafananisha.

MAELEZO

14 – Kuwa juu kwa Allaah. Kuwa juu ni miongoni mwa sifa za Allaah zilizothibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Naye yujuu kabisa, Ametukuka.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika swalah zake anapokuwa katika Sujuud:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola wangu Aliye juu kabisa.”

Ameipokea Muslim kutoka kwa Hudhayfah.

Salaf wameafikiana juu ya kumthibitishia Allaah kuwa juu. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo pasi na kupotosha, kukanusha, kuifanyia namna wala kuipigia mfano. Ni ujuu wa kikweli unaolingana na Allaah.

Kuna ujuu wa sampuli mbili:

1 – Kuwa juu kwa sifa Zake. Maana yake ni kwamba sifa Zake (Ta´ala) hazina upungufu kwa njia yoyote ile. Dalili ni yale yaliyotangulia.

2 – Kuwa juu kwa dhati Yake. Maana yake ni kwamba dhati Yake iko juu ya viumbe wote. Dalili yake – licha ya yaliyokwishatangulia – ni ifuatayo:

أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ

”Je, mnajiaminisha na Yule Aliyeko mbinguni.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola Wetu ni Allaah Aliye juu ya mbingu, limetakasika jina Lako… ”

Ameipokea Abu Daawuud na ndani yake kuna nyongeza ambayo ni ya Ibn Muhammad. al-Bukhaariy amesema:

”Hadiyth ni munkari.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah yuko wapi?” Akasema: “Juu ya mbingu.” Hivyo akasema: “Mwache huru, kwani hakika ni muumini.”

Ameipokea Muslim katika kisa cha Mu´aawiyah bin al-Hakam.

Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Huswayn bin ´Ubayd al-Khuzaa´iy – baba yake na ´Imraan bin Huswayn:

“Waache hao sita na mwabudu Yule Aliye mbinguni.”

Hili ndio tamko lililotajwa na mtunzi wa kitabu. Ameitaja katika “al-Iswaabah” katika upokezi wa Ibn Khuzaymah katika kisa kinachozungumzia kuingia kwake katika Uislamu kwa tamko lisilokuwa hili. Humo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemkubalia Huswayn pindi aliposema:

“Sita wako katika ardhi na mmoja Yuko juu mbinguni.”

Salaf wameafikiana juu ya kumthibitishia Allaah kuwa juu kwa dhati na kitendo cha kuwa Kwake juu ya mbingu. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo pasi na kupotosha, kukanusha, kuifanyia namna wala kuipigia mfano.

Ahl-ut-Ta´twiyl wamekanusha kitendo cha Allaah kuwa juu ya mbingu kwa dhati Yake na wakafasiri eti maana yake ni kwamba juu ya mbingu kuko ufalme, mamlaka Yake na mfano wake. Tunawaraddi kwa yale yaliyokwishatangulia katika kanuni ya nne. Ipo njia nyingine ya nne; ufalme wa Allaah uko juu ya mbingu na ardhini pia. Njia ya tano; dalili ya kiakili ambayo hiyo ni sifa ya ukamilifu. Njia ya tano; nayo ni ile dalili ya kimaumbile. Waja wameumbwa kwa maumbile ya kujua kuwa Allaah yuko juu ya mbingu.

[1] 67:16

[2] Abu Daawuud (3892), an-Nasaa´iy (1037), al-Haakim (1/344) na (4/218) na wengineo.

[3] Muslim (538).

[4] at-Tirmidhiy (3479), Ahmad (4/444), al-Bukhaariy katika ”at-Taariykh al-Kabiyr” (2/1/1) na wengine

[5] Abu Daawuud (4723), at-Tirmidiy (3320), Ibn Maajah (193), Ahmad (1/206), ad-Daarimiy (1/90-91), Ibn Khuzaymah katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” (68) na wengineo.

[6] 02:255

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 64-68
  • Imechapishwa: 26/10/2022