36. Baadhi ya Adhkaar baada ya kumaliza kuswali

Swali 36: Kumepokelewa mahimizo ya kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

mara kumi baada ya swalah ya Fajr na baada ya swalah ya Maghrib. Je, haya yaliyopokelewa ni Swahiyh?

Jibu: Kumepokelewa juu ya haya Hadiyth ambazo ni Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zote zinafahamisha juu ya mapendekezo ya Dhikr iliyotajwa baada ya kumaliza kuswali Fajr na baada ya kumaliza kuswali Maghrib. Nayo ni yeye kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد يحيي ويميت وهو على كل شيء قدير

“Allaah ni mkubwa. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye. Anahuisha na Anafisha. Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

mara kumi. Kwa hivyo ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa muumini wa kiume na muumini wa kike kuhifadhi jambo hilo baada ya swalah mbili zilizotajwa. Hayo yanafanyika baada ya kumaliza kuleta zile Dhikr zilizowekwa katika Shari´ah baada ya kutoa salamu katika zile swalah zote tano. Nazo ni yeye kusema baada ya kutoa salamu:

أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ، وَمِـنْكَ السَّلام، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام لا إله إلا الله، وحده لا شريك له، له الملك، وله الحمد، وهو على كل شيء قدير، لا حول ولا قوة إلا بالله، لا إله إلا الله، ولا نعبد إلا إياه، له النعمة وله الفضل وله الثناء الحسن، لا إله إلا الله مخلصين له الدين ولو كره الكافرون. اللهم لا مانع لما أعطيت ولا معطي لما منعت ولا ينفع ذا الجد منك الجد

”Namuomba Allaah msamaha, namuomba Allaah msamaha,  namuomba Allaah msamaha. Ee Allaah! Wewe ndiye as-Salaam na amani inatoka Kwako na umetukuka, Ee Mwenye utukufu na ukarimu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ufalme ni Wake na himdi zote njema ni Zake na Yeye juu ya kila jambo ni muweza.  Hapana uwezo wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, wala hatumwabudu mwengine isipokuwa Yeye, ni Zake neema, fadhilah ni Zake na ni Zake sifa zote nzuri, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kumtakasia Yeye dini, ijapokuwa watachukia makafiri. Ee Allaah! Hakuna awezaye kuzuia ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia na wala utajiri wa mtu haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako.”

Akiwa ni imamu basi imesuniwa kuwaelekea watu na awaelekezee uso wake baada ya kumaliza kusema:

أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، أَسْـتَغْفِرُ الله، اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ، وَمِـنْكَ السَّلام، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام

”Namuomba Allaah msamaha, namuomba Allaah msamaha,  namuomba Allaah msamaha. Ee Allaah! Wewe ndiye as-Salaam na amani inatoka Kwako na umetukuka, Ee Mwenye utukufu na ukarimu.”

Hivo ni kwa ajili ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jambo hilo. Inafaa kwa imamu kugeuka kwa upande wa kuliani mwake au upande wa kushotoni mwake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyafanya yote mawili.

Pia inapendeza kwa mswaliji baada ya zile swalah tano baada ya kumaliza kusoma Dhikr tulizotaja aseme:

سُـبْحانَ الله

”Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu.”

 mara 33.

الحَمْـدُ لله

”Himdi zote njema anastahiki Allaah.”

mara 33.

واللهُ أكْـبَر

”Allaah ni mkubwa.”

mara 33.

Jumla itakuwa mara tisini na tisa. Akamilishe mia kwa kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

Imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mahimizo ya kufanya hivo na kubainisha kuwa ni katika sababu ya kusamehewa.

Vilevile imewekwa katika Shari´ah kwa mswaliji baada ya kila swalah miongoni mwa zile swalah tano kusoma Aayah al-Kursiy baada ya kuleta Adhkaar hizi na asome:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم. قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Allaah ni Mmoja pekee, Mwenye kutegemewa kwa haja zote, hakuzaa na wala hakuzaliwa na wala haiwi awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye.”

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ .قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَق مِن شَرِّ مَا خَلَقَ وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ  وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Najilinda na Mola wa mapambazuko, kutokamana na shari ya alivyoviumba, na kutokamana na shari ya giza linapoingia, kutokamana na shari ya wapulizao mafundoni na kutokamana na shari ya hasidi anapohusudu.”

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ .قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ مَلِكِ النَّاسِ إِلَـٰهِ النَّاسِ مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ

”Kwa jina la Allaah, Mwingi wa kurehemu, Mwenye kurehemu. Sema: ”Najilinda na Mola wa watu, mfalme wa watu, mwabudiwa wa haki wa watu, kutokamana na shari za anayetia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma, anayetia wasiwasi nyoyoni mwa watu miongoni mwa majini na watu.”

Imesuniwa kuzikariri Suurah hizi mara tatutatu baada ya swalah ya Maghrib na baada ya swalah ya Fajr na wakati wa kulala. Kumepokelewa Hadiyth Swahiyh kuhusu hayo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 24/08/2022