Miongoni mwa ´Aqiydah na madhehebu ya Ahl-us-Sunnah ni kwamba kheri na shari vinatokana na Allaah na kwa mipango Yake. Hata hivyo haifai kukiegemeza chochote kinachopelekea kumtia Allaah mapungufu, kwa njia ya kumsifu nacho Yeye pekee. Ijapo hakuna muumba mwingine isipokuwa Mola ndiye Muumba Wake, haitakiwi kwa mtu kusema: ”Ee Muumba wa nguruwe, nyani, mende na makovu!” Kuhusiana na hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika du´aa ya ufunguzi wa swalah:

”Umebarikika na kutukuka. Shari haitokani Nawe.”[1]

Maana yake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwamba shari pekee hainasibishwi Kwako. Ingawa Allaah ndiye kaumba na kukadiria kheri na shari, haitakiwi kwa mtu kusema: ”Ee Muumba wa shari! Ee Mkadiria shari!” Kwa ajili hiyo al-Khadhir (´alayhis-Salaam) alinasibisha matakwa juu ya nafsi yake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kuwa amesema:

أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ فَأَرَدتُّ أَنْ أَعِيبَهَا وَكَانَ وَرَاءَهُم مَّلِكٌ يَأْخُذُ كُلَّ سَفِينَةٍ غَصْبًا

”Kuhusu jahazi, ilikuwa ya masikini wawili wanaofanya kazi baharini. Nikataka kuitia dosari, kwa sababu mbele yao alikuweko mfalme anayechukua kila jahazi kwa kupora.”[2]

Sambamba na hilo, wakati alipotaja kheri, wema na rehema, akaegemeza matakwa yake kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kusema:

وَكَانَ أَبُوهُمَا صَالِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَا أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ

”Baba yao alikuwa mwema, basi Mola wako akataka wafikie umri wa kupevuka na watoe hazina yao ikiwa ni rehema kutoka kwa Mola wako.”[3]

Kwa ajili hiyo Ameeleza kwamba Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ

”Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye huniponyesha.”[4]

Akaegemeza maradhi kwa nafsi yake na ponyo kwa Mola Wake, ingawa vyote vinatokana Naye.

[1] Muslim (771).

[2] 18:79

[3] 18:82

[4] 26:80

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 284-285
  • Imechapishwa: 20/12/2023