106 – ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia: “Tulikuwa tukisema wakati tunapokuwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika swalah: “as-Salaam kwa Allaah kutoka kwa waja Wake, as-Salaam kwa fulani na fulani.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Msiseme: “as-Salaam kwa Allaah, kwani hakika Allaah Yeye ndiye as-Salaam. Lakini semeni:

التحيات لله، و الصلوات و الطيبات، السلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، السلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و أشهد أن محمداً عبده و رسوله

“Maadhimisho, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah [pindi anaposema hivo basi inamgusa kila mja mwema mbinguni na ardhini]. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

Kisha achague ile du´aa inayompendeza zaidi na aombe kwayo.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

107 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitufunza Tashahhud kama anavyotufunza [Suurah katika] Qur-aan: Alikuwa akisema:

التحيات المباركات الصلوات الطيبات لله، [ال]سلام عليك أيها النبي و رحمة الله و بركاته، [ال]سلام علينا و على عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله و [أشهد]أن محمداً رسول الله

“Maadhimisho, baraka, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na [nashuhudia] ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.”[2]

Ameipokea Muslim.

108 – Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitufunza Tashahhud kama anavyotufunza [Suurah katika] Qur-aan: Alikuwa akisema:

التَّحِيَّاتُ الْمُبَارَكَاتُ الصَّلَوَاتُ الطَّيِّبَاتُ لِلَّهِ، السَّلَامُ عَلَيْكَ أَيُّهَا النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ، السَّلَامُ عَلَيْنَا وَعَلَى عِبَادِ اللَّهِ الصَّالِحِينَ، أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللهِ

”Maadhimisho, baraka, swalah na mazuri yote yanamstahikia Allaah. Amani, rehema na baraka za Allaah ziwe juu yako, ee Mtume! Amani ishuke juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”[3]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Katika Hadiyth hii kumebainishwa namna za Tashahuud ambazo zote zimewekwa katika Shari´ah. Hii ni tofauti ya aina mbalimbali inayokubalika. Inafaa kwa mswaliji kuchagua kati ya namna hizi na asizikusanye ndani ya swalah moja.

Maana ya mamkuzi ni maadhimisho. Mswaliji anaianza Tashahhud ya kwamba maadhimisho yote, sifa na utukufu yanamstahikia Allaah (Ta´ala). Utukufu na ufalme unamstahikia Allaah (Ta´ala).

Maadhimisho ni kwa Allaah maana yake ni ufalme, kustahiki na umaalum.

Swalah kumesemekana kuwa ni zile swalah tano. Kuna maoni mengine yanayosema kuwa maana yake ni maombi. Yote hayo ni ya Allaah ambaye hana mshirika.

Mazuri maana yake ni kwamba matendo na maneno yote mazuri ni ufalme wa Allaah pekee. Yanamstahikia Yeye pekee (Subhaanah).

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amani ya Allaah iwe juu yako… “

Baada ya kumsifu Mola wa walimwengu amehamia kumsifu Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mwaminifu juu ya wahy wake na mfikishaji wa ujumbe Wake. Amani imekusanya aina zote za amani. Hapa ni kumtakia amani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) duniani katika uhai wake na vivyo hivyo katika maisha yake ya ndani ya kaburi na maisha yake ya Aakhirah.

 Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… ee Mtume.”

Ni wito wa kuihudhurisha akili na sio wito wa kihakika.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Amani ishuke juu yetu… ”

Ni mafunzo kwa mswaliji ajitolee salamu yeye mwenyewe na kisha amtolee salamu kila mja ambaye ni mwema. Ni jambo limekusanya kila mja mwema aliye mbinguni na Aakhirah.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa… “

Nakiri na kutambua ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki mwingine isipokuwa Allaah. Hili ndio neno la Tawhiyd.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nashuhudia ya kwamba Muhammad… “

Nakiri na kutambua ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume wa Allaah, kwamba sio mungu, kwamba ni mtu na Mtume anayeteremshiwa wahy. Kwa hivyo yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mja na Mtume wa Allaah wa kweli hali ya kuwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwenye kuonya.

[1] al-Bukhaariy (835) na Muslim (402).

[2] Muslim (403).

[3] Muslim (404).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 105-107
  • Imechapishwa: 04/11/2025