109 – ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa ambaye amesema: “Tulikutana na Ka´b bin ´Ujrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye akasema: “Je, nisikupe zawadi niliyoisikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndio, nipe zawadi.” Akasema: “Tulimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mnaswaliwa vipi, watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani hakika Allaah ametufunza ni namna gani tukutakieni amani?” Akasema: “Semeni:

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد. اللهم بارك على محمد و على آل محمد كما باركت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa. Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa. Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، اللَّهُمَّ بَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا بَارَكْتَ عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa. Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

110 – Abu Mas´uud al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Nilijiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na sisi tukiwa katika kikao cha Sa´iyd bin ´Ubaadah. Ndipo Bashiyr bin Sa´d akasema: “Allaah (Ta´ala) ametuamrisha kukuswalia, ee Mtume wa Allaah, ni vipi tunatakiwa kukuswalia?” Akasema: “Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza hadi tukatamani asingemuuliza.” Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا بَارَكْتَ . عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ فِي الْعَالَمِينَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ، وَالسَّلَامُ كَمَا قَدْ عَلِمْتُمْ

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyowasifu jamaa zake Ibraahiym. Na mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyowabariki jamaa zake Ibraahiym katika ulimwengu kote. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”[2]

Ameipokea Muslim.

111 – Abu Humayd as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba walisema: “Ee Mtume wa Allaah, vipi tutakuswalia?” Akasema: “Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى أَزْوَاجِهِ وَذُرِّيَّتِهِ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى أَزْوَاجِهِ، وَذُرِّيَّتِهِ كَمَا بَارَكْتَ عَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ، إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ

“Ee Allaah! Msifu Muhammad na wakeze na kizazi chake kama Ulivyowasifu [jamaa zake] Ibraahiym. Na mbariki Muhammad na wakeze na kizazi chake kama Ulivyowabariki [jamaa zake] Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

عَلَى مُحَمَّدٍ وَأَزْوَاجِهِ

“… na Muhammad na kizazi chake… “

pasi na (على) sehemu zote mbili.

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim[3].

112 – Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Tulisema: “Ee Mtume wa Allaah, huku ndio kukusalimia. Tunakuswalia vipi?” Akasema: “Semeni:

اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ عَبْدِكَ وَرَسُولِكَ ، كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ، وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ ،كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَآلِ إِبْرَاهِيمَ

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, mja na Mtume Wako, kama Ulivyomsifu Ibraahiym. Na mbariki Muhammad na jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym.”[4]

Ameipokea al-Bukhaariy.

MAELEZO

Katika Hadiyth hii kunabainishwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya Tashahhud. Kuna mapokezi mbalimbali kuhusu kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mapokezi yote haya ni katika tofauti ya aina mbalimbali, kama ilivyo katika matamshi aina mbalimbali ya Tashahuud. Kwa hivyo inafaa kwa mswaliji kusoma tamko moja katika hayo na asikusanye kati ya matamshi mawili ndani ya swalah moja.

Tamko ambalo ni kamilifu zaidi la kumaswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy katika kukusanya kati ya Muhammad na jamaa zake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kuwaswalia na kuwatakia baraka, na vilevile kukusanya kati ya Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kuwaswalia na kuwatakia baraka[5].

[1] al-Bukhaariy (3370) na Muslim (406).

[2] Muslim (405).

[3] al-Bukhaariy (3369) na Muslim (407).

[4] al-Bukhaariy (6358).

[5] al-Bukhaariy (3370).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 108-110
  • Imechapishwa: 04/11/2025